………………………………………………………………..
ADELADIUS MAKWEGA,MBEYA
Disemba 16 niliwasiliana na ndugu yangu mmoja ambaye anaishi Lugoba Chalinze mkoa wa Pwani, ambaye siku hiyo nzima nilimtafuta sikumpata, lakini jioni ilipofika nilimpata na nilipomuuliza mbona alikuwa hapatikani? Ndugu yangu huyu alinijibu kuwa kwa siku nzima hiyo alienda kuwapeleka muhimbili wazazi wake ambao walikuwa na ahadi ya kumuona tabibu na kupata vipimo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Ndugu yangu huyu aliniambia kuwa ilikuwa kazi kidogo upatikanaji wake katika simu kwani aliiacha katika gari kutokana na kuhangaika na wazazi wake hao, baba yake ana miaka 82 na mama yake ana miaka 71 ambao ni watumishi umma wastaafu.
Ndugu yangu huyu alindokeza kuwa wazazi wake hawa ni walimu wastaafu, kidogo matibabu yao kwa sehemu bima ya afya inasaidia lakini kiyume na hapo mambo yangekuwa sawa na mtoto anayejifunza kuandika, herufi hapo zingekuwa kichwa chini miguu juu, zingepiga tikitaka. Kwa kuwa walitokea Lugoba, waliamka asubuhi sana na kuanza safari hiyo saa 10 alfajiri na hii iliwasaidia kufika hospitalini mapema huku wakiyapita maeneo ya Msata, Bagamoyo, Kawe na Mbezi kukiwa na kiza kinene na kweli asubuhi na mapema walikuwa wamefika Muhimbili kwa matibabu.
Walipofika hapo waliingia na kufuata utaratibu na kwa kuwa alikuwa na wazazi wawili, mama yake alienda upande anaotakiwa, huku yeye akiongozana na baba yake kwani amepata tatizo la kupoteza kumbukumbu, anahitaji mtu wa kusikiliza maelekezo ya tabibu na wakati anatumia dawa akumbushwe vizuri.
Kweli alipokuwa katika foleni, lilipokuwa likiitwa jina la baba yake kuelekea kwa tabibu, madaktari na wauguzi walikuwa wakimwambia mbona unaambatana na baba yako kila sehemu, mbona anajieleza vizuri? Kwanini usimuache yeye mwenyewe? Aliwaeleza ile shida ya baba yake ya kupoteza kumbukumbu.
Kwa kuwa walikuwa wakipata huduma hiyo Taasisi ya Jakaya Kikwete, ndugu yangu huyu ananiambia kuwa taasisi hii ni kubwa na ya mfano. Anadai kuwa ni miongoni mwa kazi kubwa alizozijenga Ndugu Jakaya Kikwete enzi ya serikali yake ya awamu ya nne.
Nilimuuliza mbona anamsifia sana Jakaya au kwa kuwa ni ndugu yake? wanatoka wote Chalinze? Alnijibu hapana, kwa kuwa yeye(huyu ndugu yangu) ni mtaalamu ya masuala ya tiba anakumbuka watu walivyokuwa wakiteseka miaka ya nyuma. Huku akitolea mfano pia ujenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma.
Ndugu huyu anasema kuwa taasisi hizo ni sawa na kuku mweupe lakini kwa sasa kumekuwa na doa jeusi katika suala la gharama za matibabu. Nilimuuliza kwani gharama zikoje? Alinijibu kuwa siku hiyo akiwa hapo wakati baba yake anachukuliwa vipimo aliisikia familia moja wakilalamika juu ya kupatikana pesa za kufanyiwa oparesheni mzazi wao aliyelazwa hapo.
Shida ambayo kwa Watanzania wengi imekuwa mwiba unawasumbua mno, anasema kuwa familia hiyo waliamua kuuza nyumba yao ili kuokoa uhai wa mzazi wao, huku wakisema kuwa nyumba siyo embe, wakijiuliza kama mteja atapatikana mara moja. Kwa meelezo ya ndugu yangu huyu anasema kuwa aliwaacha ndugu hawa wakiendelea kulijadili jambo hilo juu ya kumnusuru ndugu yao mgonjwa namna ya kupata pesa, anadai kama walipata au la pesa hizo, yeye hafahamu.
Ndugu yangu huyu kwa kuwa alipokuwa katika benchi malalamiko ya familia hii na mjadala juu ya namna ya kupata pesa ulimuhuzunisha sana, aliamua kutoka nje angalau muda uende ili baba yake apimwe haraka waondoke.
Ndugu huyu alitoka nje ya Taasisi ya Jakaya Kikwete ambapo ipo jirani sehemu ya kuhifadhia maiti ya Hospitali ya Muhimbili, anasema kuwa hapo alikaribishwa na mandhari ya ndugu waliofiwa wakienda kuchukua miili ya ndugu zao.
“Hapa niligundua jambo jipya ambalo liliniumiza zaidi ya ule mjadala wa matibabu, mtu mwingine anakuja hiace ambayo inabeba abiria, wengine malori, wengine wakija na magari ya kifahari ya kila aina kuchukua maiti hizo. Wengine wakiwa watu wengi na magari kadhaa, wengine watu wachache tu .” Aliendelea kunisimulia ndugu yangu huyu.
Akiwa nje, kwa kando alimsikia mtu mmoja akiongea na simu juu ya ndugu yake aliyefariki akisema kuwa sasa jamani changisheni pesa haraka ili mje na gari tumchukue.
“Nendeni hapo Tandika Stendi zipo hiace, ulizeni gharama yake ni kiasi gani kuubeba mwili, mimi tayari nina elfu 50,000/-.”
Alisema ndugu huyo aliyekuwa akiongea na simu.
Nilimsikiliza ndugu yangu huyu na safari yake ya Taasisi ya Jakaya nikatafakari mno akilini mwangu. Binafsi nilimwambia kuwa ni kweli Jakaya Kikwete alijenga Taasisi ya Jakaya Kikwete (yenye jina lake), Benjamini Mkapa na Mlongazila zikawekwa vifaa tiba na huduma kuanza kutolewa nia ni kusadia kupunguza adha ya kufunga safari India na ughaibuni kupata matibabu hayo.
Nilimwambia kuwa Watanzania tulio wengi ni masikini, lazima pawepo na utaratibu wa kila Mtanzania anapokuwa mgonjwa apate nafasi ya kutibiwa kwanza, pesa ije baadae. Nilimuuliza vipi kama mtu ambaye hakuwa mtumishi hali inakuwaje? Ndugu yangu huyu aliguna tu.
Katika suala la kusafirisha maiti na wagonjwa nilishauri angalau kila kata kuwa na gari la wagonjwa la umma, wananchi wao wachangie pesa ya mafuta tu kwa gharama ya chini.
Nilimwambia kuwa Ifahamike wazi kuwa yanapokuwepo magari kama haya tunajiwekewa utaratibu wa huduma hiyo sisi wenyewe kila mmoja katika maeneo yake, pale dharura inapotokea yanatumika kwa wanaohitaji.
Kwa mfano Waziri, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na hata mwananchi wa kawaida anaweza kupata tatizo vijijini au njiani kutoka eneo moja kwenda lingine, kama ambulance ipo inaweza kuokoa jahazi.
Kwa muda mrefu zinapotokea ajali ni magari ya watu binafsi na Toyota Land Kruza za Jeshi letu la Polisi ndiyo zinazotumika kubeba maiti na majeruhi, wakati si kazi yake kubeba maiti au majeruhi.
Nilipokuwa namalizia sentensi hiyo simu yangu ilikatika, maana chaji iliisha.
0717649257