Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Katavi, Nehemia James akifungua mkutano wa uhamasishaji wa utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki ambapo amesema kuwa ujio wa mfumo huo utasaidia katika kudhibiti wizi wa mifugo. Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi. (17.12.2021
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti wa Magonjwa yaenezwayo na Wadudu kutoka WMUV, Dkt. Benezeth Lutege akiwasilisha mada kuhusu mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki ambapo amewaeleza washiriki faida za matumizi ya mfumo huo. (17.12.2021)
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti wa Magonjwa yaenezwayo na Wadudu kutoka WMUV, Dkt. Benezeth Lutege akitoa ufafanuzi kwa washiriki kutokana na maswali yaliyoulizwa. Kushoto ni Afisa TEHAMA, John Ntulo. (17.12.2021)
……………………………….
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Katavi, Nehemia James amesema kuwa utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kieletroniki ni tiba ya wizi wa mifugo.
James ameyasema hayo leo (17.12.2021) wakati akifungua mkutano wa uhamasishaji wa utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambapo ameeleza kuwa kumekuwepo na tatizo kubwa la wizi wa mifugo.
Mkoa wa Katavi una jumla ya ng’ombe 6,092, mbuzi 181,296, kondoo 58,000 lakini pamoja na wingi wa mifugo hiyo, wafugaji wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la wizi wa mifugo ambapo mkoa umekuwa ukifanya jitihada mbalimbali ili kudhibiti wizi huo. Hivyo matumizi ya mfumo huu wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo ndio suluhisho sahihi litakalo dhibiti wizi wa mifugo.
“Mfumo huu wa utambuzi ndio tiba sahihi ya wizi wa mifugo lakini kwa mkoa wa Katavi pia tayari tumeshavisha hereni ng’ombe 1,036 na mbuzi pamoja na kondoo 24 lakini pia tayari tumeshatoa maelekezo kuwa mifugo yote inayoingia hapa mkoani ni lazima iwe na hereni za utambuzi,” amesema James
James ameipongeza wizara kwa uamuzi wa kuanzisha mfumo huo wa utambuzi wa mifugo na uamuzi wake wa kuanzisha kampeni ya uhamasishaji ambapo inatoa mafunzo kwa viongozi na wataalam ili waweze kuufahamu muongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti wa Magonjwa yaenezwayo na Wadudu, Dkt. Benezeth Lutege amesema kuwa suala la udhibiti wa wizi wa mifugo ni moja ya sababu ya uanzishwaji wa mfumo huo wa hereni za kielektroniki na lengo kuu ni kuwasaidia wafugaji. Lakini pia zipo faida nyingine ikiwemo ya kuwawezesha wafugaji kupata bima na mikopo.
Dkt. Lutege pia amesema kuwa wafugaji wanatakiwa kutumia hiki kipindi cha mwaka mmoja kilichotolewa na serikali kuhakikisha wanaisajili mifugo yao kwa kutumia hereni za kielektroniki kwani baada ya Agosti, 2021 hatua zitaanza kuchukuliwa kwa wafugaji ambao hawajatekeleza agizo hilo ambalo lipo kisheria.