*****************
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) leo Desemba 17,2021 ametembelea banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai ambapo amefanya ukaguzi wa awali wa maandalizi ya banda hilo kuelekea Siku ya Tanzania “Tanzania Day” kwenye Maonesho hayo itakayofanyika tarehe 26 Februari 2022 yenye lengo la kuitangaza Tanzania katika uwekezaji, utalii na biashara.
Akizungumza na Waratibu wa Ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho hayo ambao ni Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania(TanTrade) kwa Kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashiriki amewataka kuongeza kujiamini katika kuitangaza miradi ya Miundombinu ya nchi ili iweze kuvutia wawekezaji kuja kuwawekeza nchini Tanzania.
Mhe. Mkumbo amesema miradi hiyo ni kielelezo cha mazingira mazuri ya uwekezaji nchini ambapo, Tanzania inatangaza miradi ya kufua Umeme ya Mwl. Jk. Nyerere (JNHPP), reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Ujenzi wa Viwanja vya Ndege na kuimarisha usafiri wa anga.
Mhe. Mkumbo ametembelea Banda la Nchi ya Oman na Banda la Nchi ya Thailand na kufanya mazungumzo na viongozi wa mabanda hayo yaliyolenga kuvutia uwekezaji nchini.
Aidha Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) kesho tarehe 18 Desemba, 2021 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano wa kwanza wa Biashara wa (B2B) kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai unaoratibiwa na TanTrade.