Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Ummy Mwalimu akizungumza na Madiwani na watumishi wa manispaa ya Tabora ukumbi wa Isike Mwanakiyungi kushoto kwake ni Mstahiki meya wa manipaa hiyo Ramadani Kapera na kulia ni mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt Balozi Batrida Buriani.
Mkurugenzi wa manispaa ya Tabora Dkt Petter Nyanja akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizaika kwa mkutano na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Ummy Mwalimu.
………………………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Ummy Mwalimu amepiga marufuku kwa walimu kutoza fedha kiholela mashuleni na atakaye kaidi maelekezo ya serikali atachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria.
Alisema hayo jana kwenye ukumbi wa Isike Mtemi Mwanakiyungi akielekea kukagua miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali akiwa ameambana na viongozi wa mkoa na wizara ya Tamisemi .
Alisema kwamba kufanya hivyo kuna waogopesha wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shuleni kwa sababu ya michango kuwa mingi isiyokuwa ya lazima.
Waziri huyo alisema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani imedhamiria watoto wote waende shule wakapate elimu bora na sio kukaa majumbani na kufanyishwa kazi mbalimbali.
Alisema kwamba serikali imefanya jitihada za dhati kuhakikisha inatoa fedha kwa ajili ya kujenga majengo ya madarasa na ofisi ili watoto wapate elimu na baadae waweze kuwa viongozi bora.
Waziri Ummy alisema amefurahishwa na halmashauri ya Manispaa ya Tabora Kwa jitihada za kujenga madarasa 60 na halmashauri zingine mbili wameshakamilisha ujenzi wa madarasa.
Alitoa ujumbe wa mkoa wa Tabora kwamba Rais atatekeleza kazi zilizoachwa na hayati Dkt John Pombe Magufuli katika kuhakikisha watoto wote wanakwenda shule sekondari na msingi.
Aidha alisema kwamba watakaomaliza kidato cha nne katika manispaa ya Tabora ,mwaka 2021 ni 2,579 hao ndio walifanya mitihani yao.
Hata hivyo alisema kwamba Rais aliongeza fursa za kuhakikisha watoto kupata elimu na kidato cha pili watakuwa 4,922.
Kwa upandewake Mkurugenzi wa manispaa ya Tabora Dkt Petter Nyanja alimwambia waziri huyo kuwa katika hatua za kusimamia majengo ya madarasa ambayo yataweza kukidhi na kuna uwezekano mkubwa kwa kidato cha kwanza kupata nafasi.
Dkt Nyanja alisema kwamba lengo kubwa nikuboresha elimu katika maeneo yote ya manispaa ya Tabora .
Alitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha shule zinapofunguliwa ni lazima watoto wapelekwe shule nafasi zipo za kutosha katika manispaa ya Tabora.