………………………………………………….
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wameiomba serikali kuboresha utaratibu wa uzoaji taka unaoendelea hivi sasa kwa kuhakikisha taka zote zinazolewa kwa wakati kwani kumekuwepo na changamoto kadhaa zinazokwamisha maendeleo ya ukuaji wa mji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema kuwa wakala wa kampuni inayohusika na uzoaji taka kwenye vyanzo vya uzalishaji hafiki kwenye baadhi ya maeneo jambo ambalo limekuwa ni kero kwao.
Wamesema changamoto nyingine kuwa gari linalopita kuchukua taka linapita kwa mwendo kasi sana hivyo taka zinaendelea kuwepo muda mrefu hali ambayo itasababisha mlipuko wa magonjwa.
Aidha wameongeza kuwa gari hilo la uzoaji taka linapita kwa mwendo kasi na hivyo kufanya taka nyingine kutokuzolewa hali inayochangia kuwepo kwa uchafu muda mrefu na hivyo kuathiri uchumi na afya ya jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wamesema hali ni nzuri kwani taka zinazolewa kwa wakati huku wakimpongeza mkurugenzi wa Manispaa Jomaary Satura kwa kuendelea kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika Manispaa ya Shinyanga.
Kata Nne zinazopata huduma hiyo kupitia wakala wa kampuni ya Networking youth group ya Jijini Arusha ambayo inazoa taka katika kata za Ndembezi, Ngokolo, Kambarage na Shinyanga mjini ambazo zote zipo katika Manispaa ya Shinyanga.