Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na wapangaji waliopanga kwenye Nyumba za Watumishi Housing zilizopo Gezaulole Kigamboni Mkoani Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Dk Francis akisisitiza jambo kwenye mkutano wa Naibu Waziri Ndejembi na Wapangaji waliopanga kwenye Nyumba za Watumishi Housing.
Muonekano wa nyumba zilizopo kwenye mradi wa Nyumba za Wapangaji za Watumishi Housing zilizopo Gezaulole Kigamboni Mkoani Dar es Salaam.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi ( wa pili kutoka kulia) akiwa na viongozi wengine wakikagua nyumba zilizopo kwenye mradi wa Nyumba za Watumishi Housing Kigamboni.
………………………………………………………………..
NAIBU WAZIRI Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi ameutaka uongozi wa ‘Watumishi Housing’ ambao ndio wamiliki wa nyumba ambazo watumishi wa umma wamepanga kuhakikisha hadi kufikia Januari 28 mwaka 2022 wanakamilisha ujenzi wa uzio kwenye mradi wao wa nyumba uliopo Gezaulole, Kigamboni Mkoani Dar es Salaam.
Hayo ameyasema wakati alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo na kuzungumza na wapangaji wa nyumba hizo ambao ni watumishi wa umma ambapo ametatua changamoto zao zilizokua zikiwakabili pamoja na kutoa maelekezo kwa viongozi wa mradi huo kumaliza changamoto zilizobaki.
Ndejembi amesema Serikali imeweka kiasi kikubwa kwenye ujenzi wa mradi huo na lengo lake ni kutoa huduma ya makazi kwa watumishi wake hivyo kuwaagiza viongozi wa Watumishi Housing wakiongozwa na Mkurugenzi wake, Dk Fred Msemwa kuhakikisha wanamaliza changamoto zilizobaki.
” Nimekuja hapa baada ya kusikia malalamiko kutoka kwa wapangaji wa nyumba hizi ambao ni Watumishi wetu wa Umma, niuagize uongozi wa Watumishi Housing kuhakikisha changamoto zote ambazo wapangaji wamezisema ikiwemo ya Kizima Moto, ujenzi wa Ukuta na kuongeza walinzi zinatatuliwa hadi kufikia Januari 28, 2022.
“Kulikuepo na malalamiko kutoka kwa wapangaji kwamba Watumishi Housing imeshusha Kodi kwa wapangaji wapya na nyie wa zamani mnalipa kodi kubwa, niwatoe wasiwasi kodi ni ile ile ila kwa sasa Watumishi Housing wametoa punguzo la kodi kwa kipindi hiki cha Sikukuu,” Amesema Naibu Waziri Ndejembi.
Kuhusu changamoto ya kiusalama kwenye makazi hayo, Naibu Waziri Ndejembi ameagiza uongozi kuhakikisha hadi kufikia Januari 1, 2022 inaongeza idadi ya walinzi wanaolinda eneo hilo ili kuleta uhakika wa usalama wa watu na mali.