…………………………………………………………
Na John Walter-Babati
Wananchi wa Kijiji cha Luxmanda kata ya Secheda katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara wameanza ujenzi wa zahanati kwa nguvu zao ili kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu wa kutafuta huduma za matibabu.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Petro Mugitu amesema wameamua kujenga zahanati baada ya kuchoshwa na adha ya muda mrefu ya kutafuta huduma za matibabu mbali hali inayosababisha vifo vya wajawazito na watoto.
Diwani wa kata ya Secheda Ibrahim Tatook ameiomba Halmashauri ya wilaya ya Babati,serikali kuu na wadau wengine wa Maendeleo wawashike mkono ili kutimiza azma yao ya kujenga zahanati katika kijiji hicho.
Tatook amesema kuwa ujenzi huo unalenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya kijijini hapo.
Baadhi ya Wakazi wa Luxmanda wanasema wamelazimika kuanza kujenga Zahanati hiyo ili kupunguza kero wanazozipata wakati wanapotafuta huduma za afya, kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda katika Zahanati ya kijiji jirani cha Ufana au wilayani Mbulu ambapo hutumia gharama kubwa.
Emilisiana Dahfi anasema enzi zao walijifungulia katika wilaya tofauti za Hanang na Mbulu na wakina Mama wengi wamepoteza maisha kwa kujifungulia njaini kwa sababu ya umbali.
“Tunamuomba mheshimiwa Rais atukumbuke wananchi wa kata ya Secheda haswa katika kumalizia Zahanati yetu hii tulioanza, vifaa na wahudumu” alisema bi. Emilisiana
Wananchi wa kijiji hicho mbali na kujitolea kwa nguvu zao kuchimba msingi pia wamechangia shilingi Milioni 25 ambapo hadi kukamilika kwa Zahanati hiyo inatajwa kugharimu shilingi Milioni 124.