Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akifungua mkutano wa nne wa ushirikiano kati ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) ya SMT na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya SMZ, mkoani Mwanza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Bw. Gabriel Migire, akizungumza katika mkutano wa nne wa ushirikiano kati ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) ya SMT na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya SMZ uliofanyika mkoani Mwanza.
Baadhi ya wajumbe kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) ya SMT na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya SMZ, wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani) katika mkutano wao wa nne wa Watendaji Wakuu uliofanyika mkoani Mwanza.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), mara baada ya kufungua mkutano wa nne wa ushirikiano kati ya Wizara hiyo na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya SMZ uliofanyika mkoani Mwanza
PICHA NA WUU
************************
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameliagiza Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini ya Zanzibar (ZMA), kumaliza changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi na kuondoa malalamiko kwa wateja.
Prof. Mbarawa amesema hayo jijini Mwanza, wakati akifungua mkutano wa nne wa mashauriano kati ya Watendaji wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) ya Seriali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT), na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ambapo amesisitiza kushirikiana na kufanya kazi pamoja katika kusimamia sheria za usalama majini.
Aidha, Prof. Mbarawa ameshauri wataalam hao kupitia upya sheria zilizopo na kuangalia namna ya kuziboresha ili ziwiane na kutoleta mikanganyiko katika utekelezaji.
“Katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, masuala ya usafiri majini yanasimamiwa na Sheria ya Usafiri Majini Sura ya 165, Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania Sura ya 415, Sheria ya Usafiri wa Bahari ya Zanzibar Na. 5 ya mwaka 2006 na Sheria ya Mamlaka ya Usafiri Baharini ya Zanzibar Na. 3 ya mwaka 2009 hivyo uwepo wa sheria nyingi zinazosimamia suala moja unaweza kusababisha changamoto ya sheria hizo kutowiana (harmornised) wakati wa utekelezaji wake“, amefafanua Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameeleza pia umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi kwani Sekta hiyo inasaidia katika uwekezaji, kuipunguzia Serikali mzigo wa uwekezaji na vihatarishi vyake, kuongeza ajira, kuingiza fedha kwenye mzunguko, kuchangia kuleta teknolojia mpya nchini, kukuza uchumi na kuongeza pato la Taifa na fedha za kigeni.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Bw. Gabriel Migire, amesema kuwa mkutano huo utaibua fursa zilizopo kwa pande zote mbili ikiwemo ya kushirikisha Sekta Binafsi kuwekeza katika masuala ya usafiri majini/baharini ili kuhakikisha kwamba vyombo madhubuti vya usafiri majini vinapatikana katika maeneo yenye uhaba.
Bw. Migire ameongeza kuwa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kiutendaji zilizokuwa zinajitokeza kutokana na kutokukutana na kukubaliana pamoja, sasa zimepungua kwa kuwa wamekuwa wanakutana mara kwa mara na kutafuta ufumbuzi wa pamoja juu ya changamoto za kiutendaji zinazojitokeza.
Katika hatua nyingine Wajumbe hao wametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Daraja la J.P Magufuli (Kigongo – Busisi), lenye urefu wa kilometa 3.2 na kuridhishwa na maendeleo yake ikiwemo teknolojia inayotumika katika ujenzi wa daraja hilo.
Mkutano wa nne wa Mashaurino umehusishaWatendaji Wakuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi – SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ), Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Sekta ya Uchukuzi kwa upande wa SMT na SMZ na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Uchukuzi kwa upande wa SMT na SMZ.