Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Serikali imeipongeza Taasisi ya PASS TRUST kwa kubuni mfumo wa utoaji huduma ya dhamana za mikopo ya Kilimo kwa njia ya kidigitali yaani Digital Credit Guarantee.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ametoa pongezi hizo Jijini Dar es salaam leo tarehe 15 Disemba 2021 katika hafla ya uzinduzi wa utoaji wa huduma ya dhamana za mikopo ya kilimo biashara kidigitali iliyoandaliwa Taasisi ya PASS TRUST.
Waziri Mkenda amesema kuwa huduma hiyo itafungua fursa muhimu kwa wakulima, wavuvi, wafugaji na wajasiriamali mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo kuweza kushiriki katika uongezaji tija ya uzalishaji, ajira na pato la taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Wizara ya Kilimo tumejiwekea vipaumbele vya kimkakati saba (07) ambavyo ni utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu, kuimarisha huduma za ugani, umwagiliaji, masoko ya mazao, ugharamiaji wa kilimo na kilimo anga. Hivyo, jitihada hizi za PASS TRUST kuja na mfumo huu ni faraja kwetu kama Wizara kwani zinaendelea kuchagiza upatikaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za kilimo nchini.
Vilevile amesema, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itaendelea kuboresha mazingira katika ufanyaji shughuli za kilimo nchini kwa kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakati, upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi na kuendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa mazao kilimo ili kuongeza tija ya uzalishaji, kipato kwa mkulima, kuongeza ajira na pato la Taifa kwa ujumla.
“Sekta ya kilimo ni muhimu sana kwa nchi yetu kwa kuwa ndiyo inachangia asilimia 100 ya chakula chote nchini na ndiyo inayotoa ajira kwa watanzania wengi. Hata hivyo, kumekuwa na changamoto kadhaa kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa mitaji ya fedha ili kuendesha Kilimo cha kisasa na kibiashara” Amekaririwa Waziri Mkenda
“Hivyo, kwetu sisi ni Jambo la kujivunia pale tunapoona wadau wa maendeleo ya kilimo wanakuja na ubunifu unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima wetu” Amesema
Kadhalika, Prof Mkenda amesema utoaji wa huduma ya udhamini wa mikopo kidigitali utarahisisha upatikanaji wa huduma, na kuokoa gharama hivyo amewataka Watanzania wote, kutumia fursa hiyo iliyoletwa na PASS TRUST ili kuongeza tija ya uzalishaji kwenye mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya kilimo.
Amesisitiza kuwa Wizara ya Kilimo inautambua mchango wa wadau mbalimbali katika kuwezesha kufanya mageuzi ya sekta ya kilimo na kuiwezesha kuwa ya kibiashara na yenye tija kwa wakulima, wavuvi, wafugaji na taifa kwa ujumla.