Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwa katika maandamano ya Kitaaluma katika Mahafali ya 39 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Musoma mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza katika Mahafali ya 39 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Musoma mkoani Mara.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Paschal Mahenyila akielezea namna ya Chuo hicho kinavyozalisha Watalaam wa Maendeleo ya Jamii wenye kuleta mabadiliko katika jamii wakati wa Mahafali ya 39 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Musoma mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akitoa zawadi kwa mmoja wa Mwanafunzi aliyefanya vizuri katika Mahafali ya 39 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Musoma mkoani Mara.
Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Musoma mkoani Mara wakiwa katika Mahafali ya 39 Chuoni hapo.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
……………………………………………………..
Na Mwandishi Maalum Musoma Mara
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kuwa wabunifu katika utoaji wa elimu kwa wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wanaowazalisha.
Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema hayo Musoma mkoani Mara wakati wa Mahafali ya 39 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare ambapo jumla ya Wahitimu 970 wamehitimu Astashahada na Stashahada ya Maendeleo ya Jamii.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema kuwa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii viendelee kuwaunganisha wanafunzi na Wahitimu wa Vyuo hivyo na wadau mbalimbali ili waweze kutumia taaluma na ubunifu wanaoupata Vyuoni hapo ili kuwasaidia kupata uzoefu katika taaluma husika.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kusimamia Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ili viweze kutoa Taaluma yenye tija itakayowawezesha wahitimu kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizopo katika Sekta ya Ajira.
“Tutaendelea kutenga na kuleta pesa katika Vyuo vyetu vya Maendeleo ya Jamii nchini ili kuviwekea mazingira mazuri ya kuweza kutoa Taaluma ya Maendeleo ya Jamii kwa wanafunzi waliopo Vyuoni hapa ” alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Naibu Waziri Mwanaidi amevitaka pia Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kuhakikisha vinazingatia Programu ya Uanagenzi ambayo ni muhimu kwa wanafunzi wanapohitimu kwani inawasaidia kuweza kujiajiri na kuajiri wengine katika Sekta ya Maendeleo ya Jamii.
“Hii ni Programu muhimu sana kwa wahitimu kuwa wameipitia inawasaidia pale wanapohitimu waweze kuajiriwa, kujiajiri na kuajiri wengine na kusaidia kutatua changamoto za Ajira kwa vijana” alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Vilevile, amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kufanya tafiti mbalimbali zitakazotatua changamoto zinazoikabili jamii ya Watanzania kwa kupata majibu kupitia tafiti hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Musoma Paschal Mahenyila amesema kuwa wahitimu wanaotoka katika Chuo hicho wanatumika katika kuhamasisha shughuli za maendeleo kwenye maeneo tofauti katika jamii hivyo watasaidia kuleta hamasa na kuamsha Ari ya wananchi kujitolea katika shughuli za maendeleo.
“Katika kutekeleza hili la kizalisha Watalaam wa Maendeleo ya Jamii wenye viwango, Chuo kinatekeleza dhana ya ubunifu na Programu ya Uanagenzi inayowasadia wahitimu kuweza kujiajiri na kuajiri wahitimu na vijana wengine” alisema
Ameongeza kuwa kwa mwaka wa masomo 2020/2021 jumla ya wanafunzi 165 Wanawake 64 na wanaume 40 wameshiriki Programu ya Uanagenzi katika Mashirika mbalimbali mkoani Mara na Mwanza ili kuwajengea uwezo wa kuajiriwa, kujiajiri na kuajiri wengine wanapohitimu.
Aidha Paschal Mahenyila amesema kuwa Chuo katika miaka mitatu iliyopita kimefanikiwa kukarabati Majengo 6 yaliyopo Chuoni hapo na kuongeza udahili kutoka wanafunzi 618 hadi wanafunzi 970 kwa mwaka wa masomo 2021/2022 na kuanzisha Kituo cha Ubunifu Cha Kidijitali kinachosaidia kuvumbua wabunifu na kuwawezesha kujiendeleza.
Nao baadhi ya Wahitimu wamesema wanaenda kutumia Taaluma ya Maendeleo ya Jamii kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili jamii na kutafuta fursa za kukabiliana na changamoto hizo ili kuchangia katika maendeleo ya Taifa.