Watendaji kutoka taasisi mbalimbali pamoja na wanafunzi wa Shule za Msingi kutoka Wilaya ya Rufiji, Kibiti na Mkuranga wakiwa katika maandamano ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia yaliofanyika katika Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani
Afisa Miradi Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania -Dayosisi ya Mashariki na Pwani (KKKT – DMP), Msimamizi wa mradi wa Kupinga ukatili wa kijinsia kupitia jukwaa la dini mbalimbali unaotekelezwa kwa ubia na Shirika la Msaada la Norwey (Norwegian Church Aid -NCA). Bi. Agatha Lema akizungumza katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliofanyika Disemba 8 mwaka huu, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kapten Jenerali Ahemed Abas Ahemed akizungumza katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliofanyika Disemba 8 mwaka huu, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kibiti Bi. Jovitha Mulima akizungumza katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliofanyika Disemba 8 mwaka huu, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Wanafunzi katika Shule ya Msingi Bungu A, Mjawa na Jaribu Mpakani wakifanya maigizo yenye maudhui ya kupinga Ukatili wa Kijinsia katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili yaliofanyika Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
………………………………………………………….
NA NOEL RUKANUGA, PWANI.
Viongozi mbalimbali wakiwemo Wabunge na Madaiwani wametakiwa kubuni mfumo imara wa sera na sheria kwa ajili ya kuzuia ndao za utotoni, kuwalinda watoto walioolewa pamoja na kutoa mwongozo katika kutekelezaji ili kuhakikisha uwajibikaji kulingana na ilivyodhamiriwa katika ngazi ya taifa na kimataifa.
Akizungumza katika Maadhamisho ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia, yaliofanyika Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani, Afisa Miradi Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania -Dayosisi ya Mashariki na Pwani (KKKT – DMP), Msimamizi wa mradi wa Kupinga ukatili wa kijinsia kupitia jukwaa la dini mbalimbali unaotekelezwa kwa ubia na Shirika la Msaada la Norwey (Norwegian Church Aid -NCA). Bi. Agatha Lema.
Amesema kuwa wabunge na madiwani wapo katika nafasi ya kipekee ya kuendeleza na kutekeleza mfumo katika nchi pamoja na kuhakikisha sauti za wananchi zinasikika ikiwa ni pamoja na watoto wake ili waweze kuhamasisha utashi na dhamira ya kisiasa ya kukomesha ndoa za utotoni.
“Sababu za msingi ndoa za utotoni ni kutokuwepo usawa wa kijinsia na thamani ya chini wanayopewa wasichana, hali hii inaongezeka kutokana na umaskini, kukosekana usalama wa mtoto wa kike na kuwepo migogoro ndani ya ndoa” amesema Bi. Lema.
Bi. Lema ameeleza kuwa ukatili wa kijinsia unachochewa na sehemu kubwa ya kanuni zisizo sawa za kijinsia na kichangia ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Amesema kuwa ukatili umeathiri watu katika sehemu tofauti katika maisha yao ikiwemo kimwili, ki-ngono, kihisia, huku sababu nyengine zikieelezwa ni hali ngumu ya maisha, tama, wanawake kuwategemea wanaume kupita kiasia pamoja na mila na desturi.
Amefafanua kuwa katika kupambana na kukatili wa kijinsia kanisa la KKKT kwa kushirikiana na wadau maendeleo Norwegian Church (NCA) wamefanikiwa kutoa elimu katika shule za msingi za Bungu A, Mjawa na Mpakani.
Bi. Lema amesema pia wametoa elimu kwenye kamati tano za kupinga ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA), Mabaraza ya Usuluhishi katika Kata ya Bungu, Mjawa, Kibiti zilizopo Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Amesema kuwa wameendelea kukihudumia kituo cha kutoa msaada wa kisheria cha (Paralegal) Kibiti ambapo kesi nyingi wanazopokea ni migogoro ya ndoa, matunzo ya watoto, talaka, ardhi pamoja na kesi za madai.
Amesema kuwa KKT na NCA wameendelea kufanya kazi kwa karibu katika Wilaya ya Kibiti na dawani la kijinsia la Polisi, Mahakama na wanasheria wa Wilaya pamoja na madaktari katika kutoa elimu ya kijamii na makuzi kwa vijana.
“Ili kuendelea kufuchua uovu na ukatili wa kijinsia tumefanya kazi kwa karibu na vyombo mbalimbali vya vya habari ili kuendeleza mijadala kuhusu ukatili wa kijinsia” amesema Bi. Lema.
Amesema kuwa wamegundua kuna ongezeko la mimba za utotoni, ulawiti kwa wanandoa, wanafunzi wa kiume na wa kike, utelekezaji wa watoto unapelekea kwa kukosa huduma na kujiajiri katika umri mdogo.
KKKT – DMP, na NCA wanatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Utawala Bora (PETS), Uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia IT Vicoba, utoaji wa msaada wa kisheria kupitia vituo vilivyopo katika Wilaya za Kibiti, Rufiji, na Mafia na kamati za,mahusiano ya dini mbalimbali za Wilaya, kamati za wanawake na vijana.
Amebainisha kuwa kwa sasa wanatekeleza mradi wa miaka minne wa kupiga vita Ukatili wa Kijinsia kuanzia 2020 hadi 2024.
Akizungumza katika Maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kapten Jenerali Ahemed Abas Ahemed, ametoa agizo kwa Wananchi kuwa na udhubutu wa kutoa taarifa kwa Madawati ya Kijinsia pale wanapofanyiwa vitendo hivyo.
Amesema kuwa elimu juu ya ukatili wa kijinsia inayotolewa na wadau ni lazima ifanyiewe kazi, kwa kuwa kufanyiwa ukatili bila kutoa taarifa haitasaidia kukomesha vitendo hivyo.
Amewataka wanaohusika na kupokea taarifa hizo kutunza siri za watu akidai kuwa kusambaza taarifa hizo kunaweza kuchangia watu kuogopa kutoa taarifa hizo kwa kuona wanadharirishwa.
Amewashukuru wadau wote wanaofanya kazi ya kupinga ukatili wa kijinsia Wilayani humo ikiwemo Dayosisi ya Mashariki na Pwani huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano.
Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kibiti Jacob Kashinde, amewaomba wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu kukomesha vitendo vya ubakaji na mimba za utotoni ambazo zinaongezeka katika maeneo hayo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kibiti Jovitha Mulima, amesema kuwa ili kukabiliana na vitendo hivyo lazima lianze ngazi ya familia, taarifa zitolewe mapema katika madawati ili zifanyiwe kazi, wananchi wawe tayari kutoa ushahidi wanapohitajika.
Ameshauri suala la ngoma katika maeneo hilo lazima litazamwe upya licha ya kudumisha tamaduni, lakini kuna vichocheo vingi vinavyopelekea ubakaji na ulawiti kwa watoto kupitia ngoma hizo.
Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yamefanyika kimkoa wa Polisi Rufiji katika Wilaya ya Kibiti kata ya Bungu Mkoa wa Pwani, ambapo yameongozwa na kauli mbiu inayosema Mtoto wa Kike sio Bibi Arusi.