…………………………………………
Na. John Mapepele
Rais wa Jamhuri ya Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru leo Disemba 9, 2021 amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye lugha ya Kiswahili.
Rais Samia ameyasema haya jana usiku Disemba 8, 2021 jijini Dar es Salaam wakati akiwahutubia wananchi ambapo alieleza pamoja na mambo mengine mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania.
“Nchi nyingi zinatumia lugha za kigeni kama lugha za mataifa yao zinazowaunganisha, inapendeza kuona kuwa tunatimiza miaka 60 tukiwa wamoja wenye utambulisho mmoja na lugha moja ya Kiswahili inayoendelea kupata umaarufu kimataifa siku hadi siku”. Amefafanua Rais Samia.
Amesema wakati Tanzania ilipopata uhuru Kiswahili haikuwa lugha inayozungumzwa na watu wote ndani ya Tanganyika bali kizazi kilichofuata baada ya uhuru walijifunza kiswahili shuleni. Hii inafanya nchi kuwa kati ya nchi chache zenye lugha ya taifa yenye asili ya nchi husika.
Ameongeza kuwa katika miaka 60 Tanzania imefanikiwa kushawishi Kiswahili kuwa moja ya lugha rasmi zinazotumika katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Umoja wa Afrika.
Amesema, Shirika la Umoja wa Mataifa Sayansi na Elimu (UNESCO) limepitisha azimio la kutenga siku ya tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani ambapo amesema azimio hilo linaifanya lugha ya Kiswahili kuwa kuwa ya kwanza katika bara la Afrika kutambuliwa na kutengewa siku yake rasmi.
Akiongea na Waandishi wa Habari hivi karibuni, mara baada ya UNESCO kupitisha rasmi azimio hilo Waziri mwenye dhamana ya Utamaduni nchini, Mhe. Innocent Bashungwa aliwataka wadau mbalimbali wa Kiswahili nchini kuendelea kutumia lugha hiyo ili iendelee kukua duniani.