Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akisalimiana na watoto mara baada ya kumaliza mkutano wa hadhara wa kuhamasisha wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19 jana mjini Namanyele Nkasi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akizungumza na wananchi wa Namanyele wilaya ya Nkasi jana ambapo alihamasisha waendelee kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa korona.
Wananchi wa Namanyele wilaya ya Nkasi wakifuatilia matukio jana wakati wa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti kuhusu hamasa ya chanjo ya UVIKO-19.
…………………………………………………
Wananchi wa Namanyele wilaya ya Nkasi wamehamasishwa kuendelea kujitokeza kupata chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa korona ili waepuke kuambukizwa .
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti jana (06.12.2021) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kitongoji cha Posta Namanyele mjini ambapo amewaeleza wananchi hao kuwa ugonjwa wa korona unaendelea kusambaa na kusababisha vifo.
“Fanya maamuzi sasa ya kwenda kuchanja ili ujiepushe na ugonjwa wa korona ambao upo na unaendelea kuangamiza watu kote ulimwenguni. Tuchanje ili kujikinga na gojwa hili ambapo serikali imetoa chanjo bure kwa watu wote” alisema Mkirikiti.
Mkirikti aliongeza kusema pamoja na kuchanja wananchi waendelee kuchukua tahadhari ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na pia kuhakikisha mazingira yao yanakuwa safi na kula vyakula bora ili kujikinga na magonjwa mengine ya mlipuko.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Posta kata ya Isunta Namanyele Editha Msoma alisema yeye tayari amechanja na hakupata madhara yoyote hivyo akawasihi wananchi wengine kuendelea kupata chanjo hiyo inayotolewa bure kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya Nkasi.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali alisema wataalam wa afya wanaendelea kutoa huduma za chanjo ya UVIKO-19 kote wilayani humo na kuwa ni vema wananchi wakajitokeza kupata huduma hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na Shirika la Walter Reed (HJMFRI) wanaotekeleza kampeni ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata chanjo ambapo magari maaalum ya hamasa na wataalam wanapita vijijini kwa kazi hiyo.