Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza katika kilele cha mashindano ya Michezo na Sanaa ya vyuo vya ualimu UMISAVUTA yaliyofanyika kitaifa mkoani Mtwara
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa katikati akiwa ameshikilia kombe kabla ya kuwakabidhi washindi wa mchezo wa soka timu ya kanda ya mashariki katika kilele cha mashindano ya Michezo na Sanaa ya vyuo vya ualimu UMISAVUTA yaliyofanyika kitaifa mkoani Mtwara
Matukio katika Picha wakati wa katika kilele cha mashindano ya Michezo na Sanaa ya vyuo vya ualimu UMISAVUTA yaliyofanyika kitaifa uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara
……………………………………………………
Na. Projestus Binamungu,WUSM,Mtwara
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF kuwachukulia hatua waamuzi wa mpira wanao onekana kufanya mambo ya hovyo katika ligi kuu ya Tanzania inayoendelea.
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo jana Desemba 05, 2021, wakati akiongea na waandishi wa habari mkoani Mtwara katika kilele cha mashindano ya kitaifa ya Michezo na Sanaa ya vyuo vya ualimu UMISAVUTA yaliyofanyika mkoani humo kuanzia Novemba 29, 2021.
Waziri Bashungwa amesema licha ya ligi Kuu ya Tanzania kuendelea vizuri lakini kumekuwepo na waamuzi wanaofanya mambo ya hovyo ambayo siyo tu yanashusha adhi yao lakini yanavunja imani, amani na mioyoo ya wachezaji na mashabiki wa timu zinazofanyiwa mambo hayo.
“ We fikilia kuna klabu unakuta inachangishana shilingi elfu 10, au elfu tano ili hiyo klabu ikacheze sehemu fulani, inatoka Mkoa A inaenda Mkoa B alfu mwamuzi anafanya mambo ya uonevu uwanjani, hilo jambo linamuumiza si tu klabu ile ila hata yule aliyechangia elfu tano yake ili timu yake ikacheze” alisema Waziri Bashungwa.
Aliongeza kuwa “Kwahiyo inapotokea Waamuzi wachache wanataka kudhoofisha michezo kwakweli tusiwafumbie macho, Kwahiyo wito wangu kwa TFF wasipepeshe macho, wawe wakali, watumie sheria na kanuni zilizopo kuhakikisha waamuzi ambao wanafanya mambo ya hovyo kwenye viwanja, wawachukulie hatua ili tusivikatishe tama vilabu vinavyoangaika sana kupata rasilimali fedha.
Akizungumzia mashindano hayo ya UMISAVUTA Waziri Bashungwa amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Elimu pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha mahitaji ya walimu wa michezo shuleni yanaendana na uzalishaji wa walimu hao kwenye vyuo wa ualimu.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema dhamira ya kurejeshwa kwa mashindano hayo ambayo yalikuwa yamesitishwa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, ni kuwatengeneza walimu wanafunzi, kuwa imara katika michezo wenye ujuzi na uwezo wa kushiriki na kuendesha michezo katika shule watakazopangiwa pindi wanapo hitimu masomo yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Mashindano hayo kwa mwaka 2021 Doroth Mhaiki amesema matarajio yao ni kuona vyuo vya ualimu Tanzania vikishiriki katika mashindano mbalimbali ya Afrika Mashariki.
Mashindano hayo ya UMISAVUTA yameusisha Michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mpira, riadha, fani za ndani na mashindano ya ubunifu wa vifaa vya kufundishia ambapo kanda ya Mashariki imeibuka bingwa katika mchezo wa soka huku Kanda ya Ziwa ikiibuka mshindi wa jumla kwa kubeba vikombe vingi zaidi katika mashindano hayo.