Mkazi wa kijiji cha Mtowisa Sumbawanga Pilli Simwela akipata dozi ya kwanza ya chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm jana wakati wa mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuhamasisha chanjo unaofanywa kwa ushirikiano na Shirika la Walter Reed.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akitoa hamasa kwa wananchi wa kijiji cha Mtowisa wilaya ya Sumbawanga kuhusu umuhimu wa chanjo dhidi ya UVIKO-19
Afisa Afya wa Kituo cha Afya Mtowisa Plasidus Malapwa akitoa elimu ya chanjo ya UVIKO-19 kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa (hayupo pichani) jana. Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na Shirika la Walter Reed (HJFMRI) wanaendesha zoezi la hamasa na elimu ya UVIKO-19 ili wananchi wengu wajitokeze kwa wingi.
……………………………………………………….
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti amewataka wakazi wa mkoa wa Rukwa kuendelea kuchukua tahadhari ya maambukizi ya UVIKO 19 kwa kuwa ni hatari na bado upo.
Mkirikiti alitoa maelekezo hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara leo (03.12.2021) katika Kata ya Mtowisa iliyopo katika Bonde la Ziwa Rukwa katika wilaya ya Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa yupo katika ziara ya kikazi wilayani humo kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa fedha za Uviko 19 ambazo zimetolewa na Serikali kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani 2022.
Aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupata chanjo dhidi ya UVIKO 19 huku akisisitiza kuwa imethibitishwa na wataalamu wa afya kuwa ni salama.
” Msifanye mapuuza tutaangamia ,ugonjwa ni hatari jitokezeni kwa wingi mkachanje tena ni bure tutaangamia kila mtu achanje kwa hiyari yake…
” Serikali hii haiko tayari kuona nguvu kazi inateketea wakati chanjo hii sasa inapatikana jirani na wananchi… Chanjo zipo chukueni hatua kwani kinga ni bora kuliko tiba..” akisisitiza Mkirikiti.
Aliwatahadharisha waache kusikia upotoshaji wa chanjo vijiweni kwani usalama wake umethibitishwa na wataalamu wa afya na ndio maana serikali inatumia Gharama pamoja na wadau ikiwemo shirika la Walter Reed (HJMFRI) wanaendesha kampeni Vijijini kuhamasisha umma.
“Msisikie habari za kijiweni tuache poroja ,chanjo ni salama mimi pia nimechanja tuchukue hatua tusichelewa ikawa hatari. Msijikute mnalia kwa uchungu Yarabi nafsi yangu chukueni hatua sasa hivi” alitahadharisha.
Aidha aliwataka wananchi waendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizo ya UKIMWI kwa kuzingatia elimu wanayopewa pia wajitokeze kupima hali zao kila wakati.
Mwakilishi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Plasidsus Malapwa alisema chanjo ya Sinopharm inatolewa mara mbili siku 21 baada ya dozi ya kwanza ili kuimarisha kinga ya mwili.
Mkoa wa Rukwa umepokea dozi 24,123 za Sinopharm ambazo tayri zimesambazwa kote kwenye vituo vya afya ili wananchi wapate chanjo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na shirika la Walter Reed wanaendesha kampeni ya hamasa na elimu ya kujikinga na ugonjwa wa korona ikiwemo kutoa chanjo kwa wananchi ambapo magari Maalum ya hamasa yanapita Vijijini na mitaani kutoa elimu.
Mwisho.
Imeandaliwa na:
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa
MTOWISA
03.12.2021