………………………………………………………….
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Uongozi wa serikali ya Mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga umesema umeendelea kushirikiana na serikali na mamlaka zake katika jitihada za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia .
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Mtaa huo Solomon Najulwa ambaye amesema viongozi na wakazi wa mtaa huo wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Amesema kutokana na elimu sahihi waliyopatiwa wakazi wa mtaa huo kuhusu madhara ya ukatili jamii imekuwa na uelewa mkubwa kuhusu namna ya kukabiliana na matukio ya aina hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa pale inapojitokeza mtu kuhusika au kufanyiwa ukatili.
“Kama kunaukatili wowote ndani ya ngazi ya familia iwe baba anafanyiwa ukatili na mke wake avunje ukimya lakini pia kama kunawatoto ambao wapo katika ngazi ya familia ambao wanaishi maisha magumu wametelekezwa na wazazi wao na wanashindwa sehemu ya kusemea waje kwenye ofisi yangu ya serikali ya mtaa lakini pia hata kama kunajirani ameona jirani yake anafanyiwa ukatili naomba tafadhari avunje ukimya”.
“Ukatili wa kijinsia na unyanyasaji na mambo mengine mengi ambayo niya jinai sisi tunayatoa na kuyapeleka sehemu husika tunafanyakazi vizuri na jeshi letu la polisi tunafanyakazi kwa ushirikiano mzuri pamoja na vitengo vyote dawati la jinsia na watoto pamoja na ustawi wa jamii”.
Hata hivyo mwenyekiti huyo amesema pamoja na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa kama hatua ya kudhibiti ukatili lakini bado kuna viashiria vya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo mifarakano ya wanandoa ambayo imekuwa ikiathiri familia.
“Mtaa wangu umepiga hatua ya mafanikio ila bado kunaviashiria vingi kwenye familia kama vile kuna baadhi ya wazazi wanapotalakiana huziacha familia zao hasa wale watoto wasijue la kufanya na pia watoto kutawanyika hovyo na kuanza kulanda landa mtaani pamoja na kujihusisha na mambo ambayo hayana maadili”.
Serikali na wadau mbalimbali wa kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia wameendelea na maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambao kilele chake Disemba 10 mwaka huu.