Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Sita ya Kilimo Mseto yaliyoandaliwa na Shirika la Vi Agroforestry chini ya kaulimbiu ‘Kilimo mseto kwa kipato na uhifadhi wa mazingira’ leo Desemba 2, 2021 katika viwanja vya Bweri mjini Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo (mwenye tai) akisikiliza maelezo kuhusu shamba darasa la alizeti wakati wa Maonesho ya Sita ya Kilimo Mseto leo Desemba 2, 2021 katika viwanja vya Bweri mjini Musoma mkoani Mara. Wengine pichani mwenye Kaunda suti ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Sita ya Kilimo Mseto leo Desemba 2, 2021 katika viwanja vya Bweri mjini Musoma mkoani Mara.
Mkurugenzi wa Shirika la Vi Agroforestry, Bi. Eva Aberg akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Sita ya Kilimo Mseto leo Desemba 2, 2021 katika viwanja vya Bweri mjini Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo (mwenye tai) akisikiliza maelezo kuhusu jiko linalotumia nishati mbadala alipotembelea na kufungua Maonesho ya Sita ya Kilimo Mseto leo Desemba 2, 2021 katika viwanja vya Bweri mjini Musoma mkoani Mara. Wengine pichani mwenye Kaunda suti ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali na wadau wa mazingira wakati wa Maonesho ya Sita ya Kilimo Mseto leo Desemba 2, 2021 katika viwanja vya Bweri mjini Musoma mkoani Mara. Wengine pichani mwenye Kaunda suti ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi.
………………………………………………………
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo ameitaka jamii kuungana na Serikali kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kuhifadhi mazingira ikiwemo upandaji miti.
Jafo ametoa wito huo leo Desemba 2, 2021 wakati akifungua Maonesho ya Sita ya Kilimo Mseto yaliyoandaliwa na Shirika la Vi Agroforestry chini ya kaulimbiu ‘Kilimo mseto kwa kipato na uhifadhi wa mazingira’ yaliyoanza leo Desemba 2, 2021 katika viwanja vya Bweri mjini Musoma mkoani Mara.
Alisema ni vyema kila kijiji kuanzia ngazi ya kaya kikawa na utamaduni wa kupanda miti na kuitunza hatua itakayosaidia katika mapambano dhidi ya ukame na mabadiliko ya tabianchi kwa ujumla.
Akizungumza na wananchi waliokusanyika katika maonesho hayo Waziri jafo aliwapongeza wadau hao wa maendeleo na kuwataka wananchi waunge mkono juhudi za Serikali katika miradi mbalimbali inayotekelezwa ili kunusuru uharibifu wa mazingira.
“Kuna maeneo ya uwekezaji hasa hoteli hayakaliki kwa sababu kiwango cha maji kimeongezeka, visiwa Fungu kule Rufiji, Pwani limepotea, maeneo mengine ukame umeshamiri leo na maeneo mengine kukosa maji tusipochukua hatua dunia itakuwa si sehemu salama ya kuishi ndo maana na ndio maana tulifanya Mkutano wa COP26 na tuna kazi kubwa ya kufanya ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” alitahdharisha Jafo.
Aidha, alisisitiza kuwa hatuwezi kupata mabadiliko katika nchi yetu bila kuwewekeza katika rasilimali watu ili wapate ufahamu wa kutosha wa kutafsiri mambo kinadharia na kivitendo hususan katika masuala ya mazingira hivyo kuisaidia jamii.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi alisema kuwa mkoa wake umejipanga kuzindua kampeni ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali yakiwemo makazi, taasisi na vijijini.
Hapi aliongeza kuwa kupitia kampeni hiyo watahamasisha wananchi kupanda misitu kwa ajili ya matumizi ya kuni badala ya kukata miti ovyo hali inayoweza kusababisha uharibifu wa mazingira.
“Mheshimiwa Waziri tumejipanga kupanda miti kwa wingi katika mkoa wetu kupitia kampeni hii ili tuweze kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kupata hewa safi na kuondosha hewa ya ukaa,” alisema Hapi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Vi Agroforestry, Bi. Eva Aberg alisema kuwa shirika hilo linathamini mchango wa wakulima wadogo hivyo alitoa wito kwa watafiti na viwanda kufanya nao kazi bega kwa bega kupitia malighafi wanazozalisha.
Bi. Aberg alisema shirika hilo limeendelea kufanya kazi ya kutoa elimu kwa wakulima husasan katika mbinu za kilimo mseto ambacho hakiathiri mazingira ya mwanadamu.
Aliongeza kuwa kwa miaka mingi mabadiliko ya tabianchi yameleta athari kubwa kwa jamii nyingi duniani na kuwasababishia madhara hivyo alisisitiza juhudi za pamoja katika kuyakabili.