………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha , Mkoani Pwani imeeleza suala la biashara ya kujiuza inaendelea kushamiri kwa mabinti wa miaka 15 hadi 30 ,mashoga pamoja na baadhi ya wanandoa kuwa na michepuko hali inayotishia ongezeko la maambukizi mapya ya Ukimwi.
Changamoto nyingine ni ufinyu wa bajeti kwa ajili ya shughuli za kupambana na VVU na Ukimwi,uhaba wa kondomu kwa jamii ,unyanyapaa na ubaguzi unaotokana na Ukimwi na mwitiko mdogo wa wanaume katika upimaji wa VVU.
Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Siwema Cheru aliyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ,yanayofanyika Desemba 1 kila mwaka ,huku ujumbe wa mwaka huu Ni Zingatia usawa ,Tokomeza Ukimwi ,Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko, ambapo katika maadhimisho hayo ,Halmashauri ya Mji wa Kibaha imetoa vyakula na vitu kwenye kituo Cha kulelea watoto yatima Cha Shaloom kilichopo Kidenge Msangani Kibaha Mjini na upimaji afya kwa wananchi.
Cheru alieleza,kutokana na hali hiyo wamejiwekea mikakati ya kupambana na changamoto hizo na kufanya kampeni za upimaji katika maeneo hatarishi.
Alisema, Jumla ya wateja 23,961 wamepatiwa huduma ya ushauri nasaha na kupimaji VVU wakiwemo wanaume 10,481 na wanawake 13,480, waliokutwa na maambukizi ya VVU ni 861.
“Kitaifa kiwango Cha maambukizi ni 4.7 na kimkoa kimefikia 5.5 .sio hali ya kuridhika ,hivyo tunaendelea kupambana kwa kutoa elimu kwa wanaofanya biashara ya ngono, majumba ya starehe,wanaojidunga na mashoga.”alisisitiza Cheru.
Cheru alieleza kwamba,kupitia viongozi wa dini wanaendelea kutoa elimu kwa kusisitiza umuhimu wa kupima afya,suala la upatikanaji wa kondomu linafanyiwa kazi kwa ushirikiano na mfamasia wa kituo cha afya na madhara ya biashara ya ngono.
Akimwakilisha mkurugenzi, afisa maendeleo ya jamii Halmashauri ya Mji Kibaha, Leah Lwanji aliiasa jamii, wadau na wafadhili kujenga tabia ya kujitokeza kusaidia vituo vya kulelea watoto.
“Watoto wanaoishi katika Mazingira magumu wanahitaji faraja ,na kuwasaidia malezi ,hawa walioanzisha vituo vya kulelea watoto yatima wanahitaji pia kuwaunga mkono ,tusaidiane ,tulee watoto yatima Kama tunavyolea watoto wetu nao wanataka malezi bora “alieleza Leah.
Leah alisema Halmashauri hiyo ,imechangia mchele kilo 100 ,maharage, mashuka 32 ,maziwa ,unga wa ngano,maharage ,sukari,viatu na mboga mboga vyote vikiwa na gharama ya sh.milioni mbili.
Taarifa ya mgeni rasmi ,mkuu wa wilaya ya Kibaha,Sara Msafiri ilisema ,ipo kazi ya kufanya kupiga Vita janga la Ukimwi kutokana na Mji huo kukua siku hadi siku.
Nae mkurugenzi wa kituo Cha Shaloom kilichopo Kidenge, Msangani Kibaha Mjini ,Lilian Mbise alisema watoto anaowalea hadi Sasa Jumla Ni 32 wakike 17 na wakiume 15 na kituo kilianza mwaka 2016.
Lilian alitaja changamoto zinazowakabili, kuwa ni pamoja na ukosefu wa maji, upungufu wa vitanda ,makazi ambayo bado hayajakamilika ,amewaomba wadau na jamii kujitokeza kwenda kushirikiana kumsaidia kumaliza hasa ujenzi na uzio.