Na Mwandishi Wetu, Iramba
WILAYA ya Iramba mkoani Singida inatarajia kukabidhi jumla ya vyumba vya madarasa 61 ambavyo ni miradi ya elimu yenye thamani ya Sh. Bilioni 1.89 iliyojengwa kwa kutumia fedha za UVIKO 19 ifikapo tarehe Desemba 5, 2021.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Michael Matomora alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Kyengege Kata ya Kyengege.
Aidha amebainisha kwamba miradi yote imefikia hatua ya kupauliwa na tayari wasafirishaji wapo Dar es Salaam kuchukua mabati ambapo tunatarajia ndani ya siku mbili au tatu yatakuwa yamefika katika maeneo ya kazi, hivyo ni imani yetu kwamba mpaka tarehe tano tutakuwa tumemaliza kupaua kwa sababu tumesha nunua kila kitu, alisema Matomora.
Mkurungezi huyo akabainisha kwamba katika miradi hiyo 47 ni ya ujenzi wa madarasa katika Shule za Sekondari 19 ambazo zitagharimu kiasi cha sh.Milioni 940.
Aidha Mkurugenzi huyo akaeleza kwamba miradi 14 ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 14 katika shule shikizi saba (7) ambazo ni Ulongo, Magugu, Kagera, Itunda, Masunkune, Kisingu na Ibambasi ambazo zitagharimu kiasi cha Tsh. Milioni 280.
Alisema kwa ujumla Shule ambazo zinatekeleza miradi ya UVIKO 19 katika wilaya ya Iramba ni Lulumba, New Kiomboi, Kinambeu, Shelui, Kyengege, Kizaga, Kidaru, Mbelekese na Mtekente. Nyingine ni Mtoa, Tulya, Ntwike, Urughu, Ushora, Kinampanda, Mukulu, Mgongo, Kaselya na Kisiriri. alifafanua Matomora.
Akijibu baadhi ya changamoto zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo baadhi ya wakuu wa Shule kutotizimiza majukumu yao vizuri Mkuu wa Mkoa Dkt. Mahenge amesema Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote wa Serikali atakaye sababisha uzembe katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Yeyote atakayefanya uzembe wa makusudi tutamchukulia hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwakwe na wengine wenye tabia kama hizo, lengo likiwa sio kumkomoa bali ni kwa ajili ya manufaa ya jamii husika. alisema Dkt. Mahenge.
Hata hivo RC Mahenge amewapongeza viongozi wa wilaya ya Iramba kwa jitihada zao katika kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo ambapo mpaka sasa madarasa yote yamefikia hatua ya kupaliwa.
Aidha RC. Mahenge akawataka viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba pamoja na viongozi wa CCM kuendelea kusimamia kazi hizo na kuhakikisha kwamba inakamilika kabla au ndani ya Desemba 5, 2021.
Awali Suleiman Mwenda akimkaribisha Mkuu wa mkoa alisema wilaya inatekeleza miradi 47 ya ujenzi wa madarasa katika shule 19 ambapo jumla ya madarasa 18 yamefikia hatua kupauliwa katika shule saba (7)