Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt Samuel Gwamaka akitoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wachimbaji wadogo katika mgodi Mirerani Manayara
Eneo la mwekezaji mmojawapo katika kitalu B ambaye anafanya jitihada za kutunza mazingira. Mirerani Arusha
Moja ya shimo linalotumiwa na mchimbaji mdogo ndugu Elibariki Molel katika mgodi wa Mirerani Arusha
……………………………………………………..
Mkurugenzi mkuu wa Baraza la Taifa la Hifdhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt. Samuel Gwamka amewataka wachimbaji wadogo kuendelea kufanya shughuli za uchimbaji sambamba na kuzingatia taratibu za utunzaji za Mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
Ameyasema hayo katika ziara yake ya kukagua utunzaji wa mazingira katika eneo la mgodi Mirerani uliopo Mkoani Arusha ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya mazingira ili kuhakikisha mazingira yanakua safi na salama kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.
“Lengo kuu la ziara hii ni kukagua na kujiridhisha kuhusu utekelezaji wa sheria ya Mazingira ya mwaka 2004. Hii ni baada ya kuona kuwa kumekua na mabadiliko ya muda mrefu hasa baada ya kujengwa ukuta na kuwa na uchimbaji endelevu”. alisema
Ameongeza kusema kuwa baadhi ya mambo ya msingi ambayo yalilengwa kukaguliwa mgodini hapo ni pamoja na jinsi mazingira yanavyotunzwa ndani ya ukuta kwa maana ya vitalu vyote A,B,C,D na D extension.
Katika ziara hiyo tatizo kubwa la kimazingira lililooonekana ni tatizo linalohusiana na taka ngumu pamoja na taka za udongo unaotoka kwenye machimbo kutokana na kuwa na nafasi finyu kwa ajili ya kuhifadhi udongo huo.
“Changamoto hii tukiendelea kuiacha inaweza kuleta athari kubwa kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo kwa sababu udongo huu una madini ya salfa ambayo yana uwezo wa kutengeneza tindikali na hatimae inachafua vyanzo vya maji. Lakini pia wafanyakazi wanapopatwa na vumbi linalokua na graphite inawaathiri wanapata ugonjwa wa cirrhosis” alifafanua Dkt. Gwamaka
Aidha amewapongeza baadhi ya wachimbaji ambao wamejitahidi kuzingatia taratibu za utunzaji wa mazingira katika meneo ya migodi yao kwani kwa kufanya hivyo inadhihirisha kuwa wanatambua umuhimu wa kutunza mazingira.
Vilevile Dkt. Gwamaka amewahimiza na kuwaeleza wachimbaji hao juu ya umuhimu wa kufanya Tathmini ya athari kwa mazingira(TAM), kama nguzo ya kusaidia mchimbaji kuweza kutunza, kutambua athari ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi wake na namna atakavyoweza kudhibiti athari hizo ili kunusuru mzingira.
Akiongea katika ziara hiyo muwakilishi wa Mgodi wa wachimbaji hao Bwana Cartius Msosa, ameishukuru NEMC kwa ziara hiyo na pia kuelimishwa juu ya umuhimu wa kufanya tathimini ya athari kwa mazingira na ameuthibitishia umma kuwa NEMC ipo kwa ajili ya kutoa elimu juu utekelezji wa sheria ya Mazingira na sio kutoza faini. .
“Kumekuwa na mtazamo kwamba watu wa NEMC wakifika katika mgodi wanakuja kwa lengo la kutoza faini na watu wanakimbia . Mimi naomba huo mtazamo ufutike, na kila mtu afanye Tathmini ya Athari kwa mazingira katika mradi wake ni rahisi kwani inafanyika kulingana na kazi zako. Naomba watuwa NEMC wakija katika shughuli zao tusiwaogope”
Aidha, Dkt. Gwamaka amesema ipo fursa ya kutengeneza graphite kutoka kwenye udongo unaotolewa kwenye machimbo na wachimbaji wadogo. Amesema jambo hilo linaweza kupunguza mrundikano wa udongo sehemu moja na uharibifu wa mazingira.
“Ni jukumu letu wasimamizi wa sheria na watunga sera kuweza kuhamasisha uwekezaji kwenye eneo hili la Mirerani. Hii itasaidia wawekezaji kutumia udongo ambao wawekezaji wadogo wanasema ni uchafu kuleta fursa ya ajira na ya kiuchumi na kuweza kuboresha mazingira yetu na kufanya uchimbaji kuwa endelevu kwa wachimbaji”
Pamoja na hayo Dkt Gwamaka ameiomba serikali kuangalia namna ya kuweza kufikia muafaka kuhusiana na eneo la kitalu C ambacho kilisimama takribani miaka miwili bila kufanyiwa kazi. Jambo ambalo linapelekea kuharibika kwa miundo mbinu ya mgodi, serikali kupoteza mapato na uwezekano wa wachimbaji wadogo kuvamia kitalu C.
“ Lakini lipo tatizo kubwa zaidi block C eneo ambalo mpaka sasa linasimamiwa na STAMICO na Tanzanite one limesimama halifanyiwi kazi takribani miaka miwili sasa, na sisi NEMC tutaendelea kuishauri serikali kuwa block C ndio eneo pekee lililobakia ambalo kimazingira ni zuri, vilevile kuna mashafti makubwa ya Tanzanite, kwa serikali hata kwa kuingia ubia na muwekezaji yeyote mkubwa. Pia kuna miundombinu ambayo ingeweza kuwa ni mtaji kwa serikali badala yake inaoza na thamani ya mgodi inapungua. Vilevile wachimbaji wa block A na block D wanaingia chini kwa chini na kuchimba kwenda block C, tukizidi kuchelewa sana Tanzanite na graphite italiwa yote na wachimbaji wadogo. Hivyo basi NEMC kwa mamlaka tuliyonayo tutashauri mamlaka husika maamuzi yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka haraka ili kitalu C kiweze kuchimbwa kwa utaratibu ambao ni endelevu na kuleta tija katika taifa letu”
Meneja wa NEMC kanda ya kaskazini Bwana Lewis Nzali ametoa wito kwa wadau wa mazingira kuwa bega kwa bega na NEMC hususani katika swala zima la kuhamasisha wawekezaji katika kufanya Tathmini ya Athari kwa mazingira (TAM).
Naye Kaimu mkurugenzi wa Uzingatiaji Sheria na Utekelezaji kutoka NEMC Bwana Thobias Mwesiga alisema ziara hyo imekua ya mafanikio kwani maeneo yote yaliyokusudiwa ya wachimbaji wadogo na wakubwa wameyatembelea.