Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Mashauri Ndaki wa pili kulia, akimkabidhi  mifuko 150 ya saruji  Mwalimu Mkuu wa msaidizi wa shule ya msingi Sabasaba Manispaa ya Songea  Furaha Kapinga wa  pili kushoto, iliyotolewa na Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa,kulia Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Philip Beno na katikati Diwani wa kata ya Matarawe Judith Kapinga.

Diwani wa kata ya Matarawe Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Judith Kapinga kushoto akimkabidhi mifuko  150 ya  saruji Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya Msingi Sabasaba Furaha Kapinga kulia, iliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kwa ajili ya kumalizia  ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule hiyo.

Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Mashauri Ndaki kulia mstari wa chini,Afisa elimu wa mkoa huo Emmanuel Kisongo kushoto na Mkuu wa shule ya Sekondari London Ester Kulumla wakiwa  katika picha ya pomaja jana wakati Katibu Tawala alipofika katika shule hiyo kukabidhi Sh.200,000 zilizotolewa na Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kama zawadi kwa walimu hao kutokana na matokeo mazuri ya kitaaluma kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Mashauri Ndaki akizungumza na walimu wa shule ya Sekondari London kata ya Lizabon Manispaa ya Songea wakati alipokwenda kutoa zawadi ya Sh.200,000 zilizotolewa na Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kwa walimu wa shule hiyo kufuatia matokeo mazuri ya mitihani ya kidato cha sita  kwa miaka miwili mfululizo ambapo ilishika nafasi ya kwanza kimkoa,katikati Mkuu wa shule Ester Kulumla na kushoto Afisa elimu mkoa Emmanuel Kisongo.

Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Mashauri Ndaki kulia akikabidhi Sh.200,000 kwa mkuu wa shule ya sekondari London Manispaa ya Songea Ester Kulumla zilizotolewa na Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kama zawadi kwa walimu wa shule hiyo kutokana na matokeo mazuri ya mitihani ya kidato cha sita ambapo ilishika nafasi ya kwanza kimkoa.

………………………………………………………………

Na Muhidin Amri,Songea

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, ametoa zawadi ya Sh200,000 kwa walimu wa shule ya Sekondari London Manispaa ya Songea kufuatia shule hiyo kufanya vizuri katika mitahani ya kidato cha sita  kwa miaka miwili mfululizo.

Akikabidhi fedha hizo kwa niaba yake,Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Mashauri alisema, Mkuu wa mkoa amefurahishwa na juhudi zinazofanywa na walimu wa shule hiyo ambazo zimewezesha kushika nafasi ya kwanza kimkoa.

Aidha alisema, hata katika matokeo ya mtihani ya kitaifa shule ya Sekondari Londoni imekuwa miongoni mwa shule ambazo zimeshika nafasi  za juu katika matokeo ya mitihani ya kitaifa na hivyo kuutangaza vyema mkoa huo.

Alisema, Mkuu wa mkoa amefurahishwa na ufaulu wa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka 2020 ambapo zaidi ya wanafunzi 65 walichaguliwa kuendelea na masomo ya chuo kikuu.

Aidha alisema, Mkuu wa mkoa ameridhishwa  namna uongozi wa shule hiyo ulivyosimamia vizuri ujenzi wa vyumba vya madarasa na  kuwa ya kwanza katika  kutekeleza miradi ya  Covid-19 katika Manispaa ya Songea kupitia fedha za mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid -19.

Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ibuge,ametoa mifuko  ya saruji 150 kwa shule ya msingi Sabasaba kata ya Matarawe kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa.

Afisa elimu wa mkoa wa Ruvuma Emmanuel Kisongo,amewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma kwenye shule mbalimbali za msingi na sekondari mkoani humo,kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao  ili waweze kufanya vizuri katika masomo.

Alisema,suala la kuchangia chakula ni wajibu wa wazazi na walezi kwa sababu mtoto hasipopata chakula itakuwa vigumu kuelewa kile anachofundishwa na walimu na hivyo  kufanya vibaya katika masomo na mitihani.

Amewataka wazazi na walezi  kutoelewa vibaya  suala la elimu bure, kwani Serikali ina wajibu wake na wao kama wazazi wana wajibu na majukumu ya kuwapatia watoto wao mahitaji yote muhimu ikiwemo  chakula,sale na vifaa vya masomo.

Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan  kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari, ambapo  ujenzi wa  madarasa hayo utawezesha watoto wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwakani kupata nafasi katika shule watakazopangiwa.

Pia Kisongo, amempongeza Rais Samia kwa kumteua Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge  kuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kwani kwa muda mfupi tangu alipofika mkoani humo  Brigedia Jenerali Ibuge amekuwa mstari  wa mbele kusimamia suala la elimu  na  hivyo  kuwezesha mkoa huo kufanya vizuri kitaaluma.

Alisema, Jenerali Ibuge ni mfano wa kuigwa na viongozi wengine kwani amesaidia sana kuinua  sekta ya elimu kwa kutoa zawadi na motisha kwa walimu na shule mbalimbali zilizofaulisha vizuri katika mitihani mbalimbali ya kitaifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari London Ester Kulumla, amemshukuru Mkuu wa mkoa kwa kutambua juhudi za walimu wa shule hiyo katika kuhakikisha wanafunzi wanapata kile wanachostahili na wanafanya vizuri katika masomo yao.

Alisema, katika matokeo  ya mitihani ya kidato cha sita mwaka 2020 shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza kimkoa ambapo  wanafunzi 65 walipata Divisheni 1 wanafunzi 49 divisheni 2 na divisheni 3 walikuwa 11.

Alisema,hata katika matokeo ya mwaka 2021 shule hiyo iliendelea kufanya vizuri kitaaluma kwa wanafunzi 61 kupata Divisheni 1,wanafunzi 51 walipata divisheni 2 na,wanafunzi 8 walipata divisheni 3.

Amehaidi wataendelea kufanya kazi kwa bidii  na  kwa ushirikiano mkubwa, ili wanafunzi  waweze kufanya vizuri katika masomo  na mitihani ya kitaifa.