Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akiwa mtaani Buguruni kwa Mnyama jijini Dar es Salaam njiani kuelekea kwa Mzee Hussein Abdallah Stima mwanamuziki na mhasisi wa muziki wa dansi Tanzania anayesumbuliwa na maradhi ya moyo, presha na utu uzima (Hayupo Pichani).
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa waliosimama katikati akizungumza na Mzee Hussein Abdallah Stima mwanamuziki nguli na mhasisi wa muziki wa dansi Tanzania ambaye amelala chini, kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania CHAMUDATA Hassan Msumari na kulia ni Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Dkt. Emmanuel Ishengoma
Mzee Hussein Abdallah Stima mwanamuziki nguli na mhasisi wa muziki wa dansi Tanzania anayesumbuliwa na maradhi ya moyo, presha na utu uzima akiwa aemelala wakati alipotembelewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa(Hayupo Pichani)
…………………………………………………………
Na. Projestus Binamungu,WUSM
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lishirikiane na Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania,(CHAMUDATA) kumpeleka hospitali mwanamUziki mkongwe, Mzee Hussein Abdallah Stima mwenye umri wa miaka 85 anayesumbuliwa na maradhi ya moyo na presha tangu mwaka 2020 ili aweze kupata matibabu mara moja.
Mhe. Bashungwa ametoa agizo hilo leo Novemba 30, 2021 alipomtembelea Mzee Stima nyumbani kwake Buguruni kwa Mnyama jijini Dar es Salaam kumjulia hali.
“Fanyeni taratibu zote zinazohitajika haraka ili mzee wetu apatiwe matibabu, hili linawezekana”. alisisitiza Mhe. Bashungwa.
Mzee Stima ameishukuru Serikali kwa msaada huo.
Aidha, Mzee Stima ametoa wito kwa wasanii kuimba nyimbo zinazohamasisha maendeleo ya taifa na uzalendo kwa nchi yetu.
Mzee Stima ni miongoni mwa wanamuziki nguli nchini anayejulikana kwa umaridadi wake wa kupuliza saxophone unaowakosha watu wengi ikiwa ni pamoja na hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Enzi za ujana wake Mzee Stima amefanya kazi katika bendi mbalimbali ikiwa ni pamojana na Cuban Marimba, JWTZ Mwenge Jazz, Vijana Jazz, S.A. Rhumba na Washirika Njatanjata.