Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo akizungumza na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Pwani (hawapo pichani), akiwa katika ziara ya kazi wilayani Bagamoyo, mwishoni mwa juma.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (wa tatu-kulia), akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo (wa pili-kushoto), Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa (wa kwanza-kushoto) na wataalam kutoka REA na TANESCO, wakati Ujumbe huo ulipokuwa katika ziara ya kazi wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, mwishoni mwa juma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo akiwa amefuatana na Mjumbe wa Bodi, Oswald Urassa, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy, watalaam kutoka REA na TANESCO pmaoja na mkandarasi kutoka kampuni ya Sinotec, wakikagua mradi wa kusambaza umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa miji, Kitongoji cha Dagaza wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani mwishoni mwa juma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (katikati), Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (kulia), wakiwa katika kikao na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Pwani (hawapo pichani). Viongozi hao walikuwa katika ziara ya kazi wilayani Bagamoyo, mwishoni mwa juma.
Msimamizi wa miradi ya umeme vijijini, Kanda ya Mashariki, Mhandisi Balisidya Myula akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo, Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (hawapo pichani). Viongozi hao walikuwa katika ziara ya kazi mkoani Pwani, mwishoni mwa juma.
Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini Mkoa wa Pwani, wakiwa katika kikao na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo, Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (hawapo pichani). Viongozi wa REA walikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, mwishoni mwa juma.
******************************
Na Veronica Simba, REA – Pwani
Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini wametakiwa kuandaa mpango kazi unaoainisha kazi zote wanazofanya pamoja na muda wa kuzikamilisha kwa kila hatua.
Sambamba na hilo, wameagizwa kila mmoja kuwasilisha mpango kazi wake kwa viongozi wa eneo anakotekeleza Mradi akiwemo Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mbunge, Diwani, Mwenyekiti wa Kijiji na Ofisi ya TANESCO ili kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa juma na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo, ambaye alifuatana na Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Hassan Saidy, wakiwa katika ziara ya kazi wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
“Hili ni agizo kwa wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote. Kila mmoja awasilishe mpango kazi wake kuanzia sasa hadi pale mradi utakapokamilika,” alisisitiza Wakili Kalolo.
Vilevile, Ujumbe huo wa REA ulitoa maagizo kwa wakandarasi kuhakikisha wanajenga uhusiano mzuri na jamii katika maeneo wanakotekeleza miradi.
Akifafanua kuhusu agizo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa REA aliwataka wakandarasi kuwaelekeza wafanyakazi na vibarua wao kutumia lugha nzuri wakati wakiwasiliana na jamii, kulipia kwa wakati huduma zote zinazotolewa na wananchi pamoja na kujiepusha na vitendo mbalimbali vilivyo kinyume na maadili ikiwemo mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi pamoja na mabinti wadogo.
Aidha, viongozi hao waliwaelekeza wakandarasi kuhakikisha wanatumia vifaa vyenye ubora katika kutekeleza miradi hiyo kwani serikali haitahusika kulipia gharama ya kubadili vifaa vitakavyokaguliwa na kuthibitika kuwa havina ubora unaotakiwa.
“Mkandarasi atakayeagiza na kutumia vifaa visivyo na ubora, atambue kuwa atabeba gharama ya kuvibadilisha,” alisisitiza Mhandisi Saidy.
Naye Mjumbe wa Bodi, Oswald Urassa aliwasisitiza wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha miradi wanayotekeleza kwa muda ulioafikiwa katika mikataba yao na kuongeza kuwa wazingatie ubora unaotakiwa.
“Wakandarasi wakumbuke kuwa hatutaongeza muda wa kukamilisha miradi hiyo hivyo wajipange kwelikweli,” alisema Urassa.
Katika hatua nyingine, viongozi hao wa REA waliwaasa wananchi kutunza miundombinu ya umeme iliyopo katika maeneo yao kwani serikali inatumia fedha nyingi kuijenga, hivyo uharibifu wake ni hasara kwa serikali na wananchi wa eneo husika.
Katika ziara hiyo, viongozi hao walikagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini wilayani Bagamoyo, hususan mradi wa kusambaza umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa miji maarufu kama mradi wa Peri-Urban.
Pia, walifanya kikao pamoja na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Pwani na kujadiliana maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kutoa maelekezo yanayohusu ukamilishwaji wake kwa wakati.