……………………………………………………………………
Wizara ya Viwanda na Biashara imeshiriki katika Maonesho ya Mawasiliano, Utalii, Utamaduni na Biashara yanayofanyika katika viwanja vya Malamala kata ya Igoma mkoani Mwanza.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu Mawasiliano ni Msingi wa Uchumi, Je Umewasiliana yamefunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel.
Mhandisi Gabriel amepongeza taasisi zote za serikali na sizizo za Serikali kwa kushiriki katika kutoa elimu ya shughuli wanazofanya na huduma wanazotoa kwa wananchi.
Aidha Mhandisi Gabriel amefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kuwapa elimu ya biashara na kuwajengea uwezo wajasiriamali kubuni na kuzalisha bidhaa mbalimbali ambapo uzalishaji wa bidhaa hizo unapunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
“Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia SIDO imekuwa ikishiriki katika kutoa Elimu kwa wajasiriliamali wetu hapa nchini na kuwajengea uelewa mkubwa wa kufanya Biashara katika Mazingira mbalimbali ya nchi yetu. Amesema Mhandisi Gabriel.
Maonesho hayo yaliyoanza rasmi tarehe 23 Novemba, 2021 yanatarajiwa kumalizika tarehe 2 Desemba, 2021 ambapo maonesho hayo ni mwendelezo wa shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa nchi yetu.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amepata fursa ya kutembelea banda la Wizara ya Viwanda na Biashara na kusisitiza kwa Wizara kutumia muda wa maonesho kutoa elimu zaidi kwa vijana wazawa ili kuwajengea morali ya uzalendo itakayolisaidia taifa siku za usoni.
Maonesho haya yametembelewa na wageni na Viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka ndani na Nje ya Mkoa wa Mwanza ambapo maafisa waiopo katika banda la Wizara wameshiriki kikamilifu katika kutoa elimu ya Sera na Mikakati inayosimamiwa na Wizara katika kuelekea uchumi wa Viwanda.
Aidha, banda la Wizara limetembelewa na wageni wakiwemo wanafunzi kutoka shule ya sekondari Shamaliwa na kuelezwa majukumu mbalimbali yanayofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara.