******************************
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, amewataka wadau, wapenzi na wataalamu wa lugha aushi, adhimu na adimu ya Kiswahili, kujiandaa na kutoa maoni yao wakati huu ambapo Kiswahili kimetangazwa kikiwa moja ya lugha kubwa kuadhimishwa kidunia kuanzia Julai 7 mwakani.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo jijini Tanga alipokuwa akifungua Kongamano la Kiswahili, Utamaduni na Utalii lililoandaliwa na Shirika la Urithi wa Utamaduni wa Kiswahili (SUUKI) la jijini Tanga. Hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Majestic Cinema.
“Tanga na ukanda wote huu wa Pwani kutoka Manzabay mpaka Moabay ni moja ya kitovu kikubwa cha Kiswahili na utamaduni wa Kiswahili ndio maana mliponialika, licha ya shughuli nyingi na mnajua leo tunafungua mashindano ya soka Afrika kwa walemavu, kule wizarani tukakubaliana kugawana majukumu. Lakini pia mimi asili yangu ni huku hivyo nimekuja pia kutimiza fasalsa ya methali ya Kiswahili isemayo: ‘Mwenda Tezi na Omo, Marejeo Ngamani.,” alisema Dkt. Abbasi na kuongeza;
“Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imepania kuenzi lugha yetu ya Kiswahili na kuanzia mwakani kama UNESCO walivyotupa heshima Tanzania itaiongoza dunia kuratibu vyema maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Dunia kutokea hapa nchini ili dunia ijue kwamba Kiswahili kinanasaba kubwa na nchi yetu na hususani Tanga.”
Dkt. Abbasi pia amewataka wadau hao kuwasilisha mapendekezo yao Serikalini ili yafanyiwe kazi kuhakikisha utamaduni wetu ikiwemo lugha ya Kiswahili vinaenziwa na kuwa sehemu muhimu ya kuvutia watalii.