Alhaji Abubakar Athuman, akiwaonyesha waandishi wa habari eneo lake lililotwaliwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza bila kumlipa fidia.
Alhaji Abubakar Athuman (kushoto) akielekea kwenye jengo la mradi wa LVRLAC lililojengwa kwenye shamba lake kwa maaelekezo ya Jiji la Mwanza.
Akiwaonyesha waandishi wa habari baadhi ya miti iliyokatwa kwenye shamba lake.
Alhaji Abubakar Athuman, akihojiwa n baadhi ya waandishi wa habari akiwa kwenye eneo lake analodai kuchukuliwa na Jiji bila fidia. Picha na Baltazar Mashaka
……………………………………………………….
BALTAZAR MASHAKA , MWANZA
Mgogoro wa malipo ya fidia ya ardhi uliofichwa na wataalamu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji kwa miaka 11 iliyopita, umeibuliwa wiki iliyopita kwenye kikao cha Bazara la Madiwani la Halmashauri hiyo.
Usiri wa mgororo huo uliibuliwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Mipango Miji na Mazingira,Hamidu Selemani,akihoji shughuli zipi zinazofanywa na wataalamu wa halmashauri madiwani hawapaswi kuzifahamu.
Diwani huyo wa Kata ya Mirongo kabla ya kujibiwa alihoji kwa nini madiwani hawajawahi kuambiwa mgogoro wa malipo ya fidia ya eneo la bustani ya Tamperre hadi waliponusurika kupigwa na wananchi walipotembelea hilo.
“Kwa nini kuwe na usiri wa mgogoro huo wakati watendaji mnafahamu sisi madiwani tupaswa kufahamu na juzi nusura tupigwe na wananchi tulipotembelea eneo hilo, kumbe kulikuwa na kesi watu hawajalipwa fedha zao za fidia,”alieleza Seleman.
Mkurugenzi wa Jiji,Sekiete Yahaya,alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kusema hakuna shughuli inayopaswa kufanyika kwenye halmashauri bila madiwani kufahamishwa na suala wajumbe wa kamati ya mipango miji kunusurika kupigwa ndio analisikia.
Wakati hayo yakijiri kwenye baraza hilo mmiliki wa eneo hilo,Alhaji Abubakar Athuman (82) mkazi wa Mtaa wa Riverside, wilayani Nyamagana,ameiangukia Serikali ya Awamu ya Sita,akiomba imsaidie kupata haki yake baada ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza,kushindwa kumlipa fidia ya kutwaa ardhi na kuharibu mali zake.
Kikongwe huyo alisema halmashauri hiyo ilitwaa eneo hilo la Tamperre analolimiliki kihalali kwa miaka 45 baada ya kulinunua mwaka 1976 kwa mwanajeshi mstaafu wa JWTZ, Hebroni Mwampodere kwa sh. 2,500,sasa linatarajiwa kufanywa bustani ya kupumzikia.
Alilalamika kuwa jiji linataka kujinufaisha kwa ardhi yake kinyume cha sheria,kwa kumpora eneo hilo na kummilikisha mtu mwingine (hakumutaja) bila kumlipa fidia ya ardhi na uharibifu wa mali (miti ya matunda,mbao,migomba,mihogo na miwa)na kumwita mvamizi.
Alhaji Athuman, alisema kwa umri wake mkubwa na uwezo mdogo wa kiuchumi, hana namna ya kumudu kupambana na jiji waliotwaa ardhi yake zaidi ya kuomba msaada kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amedhihirisha ni kimbilio la wanyonge hataki dhuluma wala kupora mali watu.
Alisema amehangaika kudai haki yake tangu mwaka 2010 bila mafanikio baada ya waliopewa dhamana na serikali kufanya uthamini wa miti ya matunda, mbao na migomba,kukataa kumlipa fidia ya sh.bilioni 1.447 na ndio sababu anamwomba Rais Samia kuingilia kati amsaidie kupata haki yake.
Kikongwe huyo alisema Mthamini wa Jiji la Mwanza,Ramadhan K.S. alifanya uthamini wa miti iliyokuwa kwenye shamba hilo Novemba 11,2010 kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Namba 4 ya 1999 ya Miji na Sheria ya Namba 5 ya 1999 ya Vijiji na kuonyesha anastahili fidia ya sh. 1.447,133,130.60.
Akionyesha masikitiko yake baada ya kutolipwa alifungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza lakini hakuridhika na hukumu iliyotolewa na Jaji Matupa,kuwa alipwe kiwango hicho cha fedha kilichothaminiwa na mshitakiwa wa kwanza kwenye shauri hilo ambaye alipewa kazi na jiji, kujenga ofisi kwenye eneo lake la Tamperre.
“Sikuridhika na hukumu hiyo nimekata rufaa kwa sababu mtu aliyehukumiwa kunilipa hizo sh.1,447,130,133.60, jiji lilimkana mahakamani,wakati lilimpa kazi ya kujenga nyumba ya ofisi ya Mradi wa Lake Victoria Regional Local Authorities Cooperation (LVRLAC) licha ya kutoa vielelezo vya mikataba ya kazi,” alisema Alhaji Athuman.
Alieleza kuwa anasikitika wakati bado shauri la rufaa namba 35/2015 liko Mahakama Kuu Mwanza,uongozi wa Jiji umesimika vigingi kwenye shamba lake hilo bila fidia yoyote ambapo mwanzoni mwa mwezi huu jiji waliharibu tena miti ya matunda na mbao iliyooteshwa kwenye eneo hilo.
“Nimeleta kilio changu kwa Mkuu wa Nchi,Rais Samia Suluhu Hassan,anisaidie kupata haki yangu naamini ni msikivu asiyependa dhuluma,iweje mtu aliyepewa kazi na jiji awajibike kunilipa haki zangu? Ili kuficha ubaya walioufanya wamegeuka na kuniita mvamizi kwenye ardhi yangu, ndiyo maana namwomba Rais anisaidie,”alisema.
Aidha Daud Lyakugwile anayedaiwa kukata miti kwenye shamba la alhaji Athuman kwa maelekezo ya uongozi wa Jiji la Mwanza,akizungumzia mgogoro huo alikiri kupewa kazi na maofisa wa jiji hilo,kujenga jengo la Mradi wa LVRLAC.
Alisema jengo hilo alilijenga Agosti 2006 kwa gharama ya sh.milioni 10.2 kabla ya uthamini kufanyika,fedha ambazo hakulipwa hadi leo na baadaye alishitakiwa mahakamani kwa kuvamia na kuharibu mali ya Alhaji Abubakar Athuman.
“Wahusika walionipa kazi ni Eric Nyoka na Patrick Karangwa kwa niaba ya Jiji la Mwanza,baada ya kulikamilisha jengo waliendelea kulitumia hadi nilipofunguliwa kesi ya kuharibu mali wakanikana ingawa ushahidi wa mkataba na vitabu vya site ulionyesha ni waajiri wangu, pia bado nina haki zangu naidai Halmashauri ya Jiji fedha za jengo la mradi wa LVRLAC,”alisema Lyakugwile.