Uzinduzi rasmi wa kifurushi kinachojulikana kwa jina la ‘BUFEE PACK’ ukiendelea katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam. |
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) limezinduwa huduma mpya, ya kifurushi kinachojulikana kwa jina la ‘BUFEE PACK’. Kifurushi hicho maalum kama zawadi kwa wateja wa mtandao wa TTCL kuelekea siku kuu za mwisho wa mwaka kinampa mteja fursa ya kujichagulia kiwango cha muda wa maongezi, huduma ya data na ujumbe mfupi kulingana na mahitaji yake.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL Corporation, Bw. Vedastus Mwita amesema katika huduma hiyo mpya ya mteja kujichagulia kifurushi kulingana na mahitaji yake, TTCL imekuja kivingine huku lengo likiwa ni kuleta FURAHA na TABASAMU kwa wateja.
“Safari hii tumekuja kivingine kabisa kwa kumpa mteja fursa zaidi ya kujitengenezea kifurushi chake mwenyewe kadri ya mahitaji yake ya Dakika, SMS na Data kwa gharama nafuu zaidi. Mteja ataingia kwenye menyu *148*30# kisha atachagua namba 6, mteja atapaswa kufuata maelekezo.
Alisema kwa kumjali mteja wao zaidi, Kifurushi cha BUFEE kitakuwa hakina UKOMO wa Muda hivyo atatumia kifurushi chake mpaka kitakapoisha kabisa huku akipewa taarifa kulingana na matumizi.
“Hivyo, tunapenda kuwakaribisha wateja wote kutumia fursa hii ya uwepo wa kifurushi cha BUFEE ili waweze kufuruhia mapumziko ya mwaka wakiwa na Data, SMS na Intaneti yenye kasi zaidi kwa gharama nafuu zaidi,” aliongeza Bw. Mwita.
Aidha alisema TTCL Corporation inapenda kuwashukuru wateja wake ambao wamekuwa wadau muhimu katika kulikuza na kuliletea maendeleo Shirika na kuahidi wataendelea kuwaletea huduma nzuri na nafuu kwa mteja ikiwa ni kutambua mchango wao.
TTCL inatambua kuwa tupo katika msimu wa Siku Kuu za mwisho wa mwaka hivyo tumeona sasa ni muda muafaka wa kuwarahisishia huduma za mawasiliano hivyo kuwapa tabasamu wateja kwa kifurushi cha kujipimia mwenyewe.
“tunambua umuhimu wa siku kuu hizi, Shirika tumependelea kuwajali wateja wetu, tunafahamu ni kipindi ambacho wateja na watanzania kwa ujumla wanaenda mapumziko ya mwaka,” alibainisha Mkurugenzi huyo wa Biashara wa TTCL Corporation akiwaeleza wanahabari.
Pamoja na hayo alisema kuwa TTCL inatambua kuwa Taifa lipo katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, hivyo kifurushi hicho kitakuwa kama faraja kubwa kwa Taifa kufikisha miaka 60 likiwa Taifa moja lenye Amani, Ushirikinano na Umoja, huku wakifurahia matunda ya uhuru.
“Miaka 60 ya Uhuru sekta ya Mawasiliano imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwani sasa Watanzania wanatumia huduma za simu kwa gharama nafuu na zenye uhakika, mawasiliano yanapatikana vijijini na mijini. Kama Shirika tumekuwa na mchango mkubwa katika kukuza matumizi ya TEHAMA na sekta ya mawasiliano kwa ujumla.”