Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Baraza hili la siku mbili linafanyika Mkoani Mwanza. Akifungua Baraza hilo, Mhe. Pinda amesema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni nguzo na mhimili wa uendeshaji wa Serikali na ina dhamana kubwa.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt Eliezer Feleshi akimkaribisha Mgeni Rasmi Naibu Waziri Mhe. Geophrey Pinda kufungua Baraza la Wafanyakazi ambapo pamoja na mambo mengine, amesema Ofisi yake haitamvumilia Mtumishi atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa
………………………………………………………..
Na Mwandishi Maalum,Mwanza
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Mizengo Pinda amewataka Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutambua uzito na dhamana ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika uendeshaji wa Serikali.
Ameyasema hayo leo ( Jumanne) Wakati alipokuwa akifungua Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Baraza hilo linafanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jengo la TMDA Mkoani Mwanza.
Akasema, kwa mujibu wa Majukumu ambayo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepewa Kikatiba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ni nguzo na mhimili wa uendeshaji wa Serikali na kwamba ufanisi wa serikali kwenye masuala ya kisheria unawategemea sana watumishi wa Ofisi hiyo.
“Kwa muktadha huu, ni vema mtambue kuwa mmpewa majukumu nyeti, na mmebeba dhamana kubwa ya kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake, na nyinyi ndiyo taswira ya Taifa letu kwenye masuala ya Utawala na Sheria” amesisitiza Naibu Waziri Pinda.
Aidha ametoa rai kwa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kwamba wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu wa kiwango cha juu na kwa maslahi mapana ya nchi.
“Kwa kufanya hivyo mtaiwezesha Serikali kupata ushindi kwenye kesi nyingi na kupunguza migogoro ya kisheria baina ya Serikali na Wabia” amebainisha Naibu Waziri.
Katika Baraza hili la Wafanyakazi ambalo Mwenyekiti wake ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Eliezer Feleshi, Naibu Waziri Pinda pia ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuendeleza juhudi za Serikali za kuondokana na Sheria zenye mianya ya rushwa kwa kuandaa Mikataba yenye tija na inayozingatia maslahi ya Taifa.
Vile vile Naibu Waziri Pinda amesisitiza watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuvitambua vipaumbele vya Serikali ya awamu ya Sita na jinsi gani vipaumbele hivyo vinatekelezwa kwa kuzingatia majukumu ya Ofisi.
Pamoja na kusisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika utoaji haki, pia amesisitiza umuhimu kwa watumishi kuzingatia Sheria, Kanuni na miongozo ya kiutumishi na kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo wa kufutailia utendaji wa wanasheria wote wa Serikali na mpango wa Mawakili wote kupata uzoefu wa kazi mahakamani.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Katiba na Sheria kufungua mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Eliezer Feleshi, amesema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa.
“ katika eneo hili la uadilifu, niwasihi watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Muu wa Serikali mnatakiwa kutekeleza majukumu yenu ya kazi kwa kuzingatia Maadili ya Utumishi wa Umma, Sheria na Kanuni. Mla rushwa hata vumiliwa hata kidogo” akaonya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kuhusu idadi ya watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Feleshi amesema kwa mujibu wa Muundo wa Ofisi, Ofisi inahitaji kuwa na watumishi 477 ili kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika mikoa yote 26.
“Mhe Naibu Waziri watumishi waliopo sasa ni 121,kati hao Mawakili wa Serikali ni 54 na watumishi wa kada nyingine ni 67, idadi hii ya watumishi hasa Mawakili wa serikali ni ndogo sana ikilinganishwa na mahitaji ya mawakili wa Serikali 241 wanaohitajika kutokana na kuongezeka kwa majukumu ya Ofisi katika maeneo ya upekuzi wa mikataba, Uratibu wa Huduma za Ushauri wa Kisheria na Uandishi wa Sheria.
Dkt, Feleshi amesema Ofisi imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuongeza watumishi kwa kutenga nafasi za uhamisho na ajira mpya kwenye Ikama kila mwaka na kuwasilisha Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwa Hatua zaidi.
Amebainisha kwamba suala la uhaba wa watumishi haupo tu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bali pia ni tatizo ambalo pia linazikabili Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na kwamba zoezi la kukamilisha uchambuzi wa mahitaji ya watumishi kufuatia mahitaji halisi ya huduma za kisheria zintolewazo na ofisi hizo kwa mujibu wa Katiba na Sheria ili kwenda na mgawanyo wa maeneo ya kiutawala Serikalini.
Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unahudhuriwa na Wanachama 45 wa TUGHE pamoja na wajumbe waalikwa wakiwamo mawakili wa Serikali wanaosimamia Ofisi za Tabora, Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro ,Mbeya, Mtwara na Kagera.