Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akizungumza mara baada ya ukaguzi wa mradi wa maji wa Kigamboni.
Tenki lenye ujazo wa lita za maji milioni 15 mradi wa maji Kigamboni.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akipata maelezo ya mradi wa maji Kigamboni
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza mara baada ya ukaguzi wa mradi
………………………………………………………………
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewataka wananchi na wakazi wa jiji la Dar es salaam na mkoa wa Pwani kuhakikisha wanatumia maji kwa uangalifu na kujiepusha na matumizi yasiyo ya lazima. Ametoa kauli hiyo wakati akikagua hali ya utekelezaji wa mradi wa maji Kigamboni.
Amesema Wizara ya Maji inaendelea na zoezi maalumu la kuhakikisha uchepushaji wa maji pamoja na shughuli mbalimbali za kibinadamu ambazo zinaathiri upatikanaji wa maji kwa wananchi zinakomeshwa.
“Niwahakikishie wananchi wa Jiji la Dar es saalam na wale wa mkoa wa Pwani. Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Dar es Salaam (DAWASA) tunaendelea na zoezi la kuzuia uchepushwaji wa maji katika vyanzo vyetu vya maji, pia kuzuia shughuli za kibinadamu katika kuhakikisha maji hayo yanaingia katika mzunguko wa huduma kwa wananchi kwa kusukumwa katika mitambo yetu ya Ruvu. Niwaombe wananchi wasiwe na taharuki. Hiki ni kipindi cha mpito. Haya yatapita na Mungu wetu ni mwema sana. Atatuvusha salama. …Niwaombe sana. Hakikisheni mnatunza maji. Matumizi ya maji yasiyokuwa ya lazima tuepukane nayo.” Waziri Aweso amesema.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema shughuli za utekelezaji wa mradi wa maji Kigamboni unakwenda vizuri.
“Tumemuagiza mkandarasi ahakikishe anakamilisha kazi hii kwa wakati. Tenki hili lenye ujazo la lita milioni 15 litakuwa limekamilika mwishoni mwezi wa 12 mwaka huu.” Amesema Mhandisi Luhemeja
Kukamilika kwa mradi wa maji Kigamboni kutawezesha upatikanaji wa lita za maji milioni 57 kwa siku. Mahitaji ya maji kwa mji wa Kigamboni kwa sasa ni lita Milioni 24 kwa siku.