Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza jambo baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Bukoba kwa ajili ya kufanya ziara ya siku mbili mkoani Kagera ambapo amepokelewa na viongozi na wataalam kutoka Sekta ya Uvuvi wakiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi, Bw. Ezra Mutagwaba (wa pili kutoka kulia).
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Ntangeki (kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) kuhusu ujenzi unaoendelea wa Kiwanda cha kutengeneza Chakula cha Mifugo pamoja na kiwanda cha maziwa kinachojengwa katika Kijiji cha Kihanga wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiwa kwenye moja ya shamba la malisho ya mifugo linalomilikiwa na Kampuni ya Kahama Fresh ambapo ameendelea kuwahimiza wawekezaji wengine kujenga tabia ya kupanda malisho kwa ajili ya mifugo yao. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Ntangeki na wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Karagwe, Ndg. Pascal Rwamgata.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiwaangalia ng’ombe waliokuwa wanatoka kuogeshwa kwenye moja ya josho linalotumia mashine katika moja ya Kitalu cha NARCO kinachotumiwa na Kampuni ya Kahama Fresh kilichopo wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.
Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) na Viongozi na Wataalam kutoka WMUV, Chama cha Mapinduzi na baadhi ya wawekezaji mara baada ya kumaliza kutembelea mifugo inayomilikiwa na Kampuni ya Kahama Fresh. Mhe. Ulega amempongeza Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bw. Josam Ntangeki kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kupitia sekta ya mifugo.
…………………………………………………….
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wafugaji hapa nchini kulima malisho kwa ajili ya mifugo yao.
Naibu Waziri Ulega ameyasema hayo wakati alipotembelea shamba la malisho ya mifugo kwenye kitalu cha NARCO ambacho kinatumiwa na Kampuni ya Kahama Fresh wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.
Akiwa katika shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 400, Naibu Waziri Ulega amesema wafugaji wanatakiwa kulima malisho na kuacha kutegemea malisho ya asili peke yake. Lakini pia amesema ipo fursa kubwa kupitia kilimo cha malisho kwa wafugaji na wasio wafugaji kwani kufanya biashara ya malisho ya mifugo kutawawezesha kujinyanyua kiuchumi.
Naibu Waziri Ulega ametembelea kuona ujenzi unaoendelea wa kiwanda cha vyakula vya mifugo pamoja na kiwanda cha maziwa, ambapo ameipongeza Kampuni ya Kahama Fresh kwa kuamua kufanya uwekezaji huo. Vilevile ametembelea kuona mifugo inayomilikiwa na Kampuni hiyo ambapo amesema kuwa mwekezaji huyo ameonesha mfano mzuri wa matumizi ya ardhi aliyokodoshiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kuwataka wawekezaji wengine kufuata taratibu wanazopewa.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Ntangeki amesema kwa upande wa kiwanda wanatarajia kiwe kimekamilika ifikapo mwezi Machi, 2021. Lakini kwa sasa wanaendeleo kutoa mitamba kwa ajili ya maziwa kwa wafugaji wadogo ambao ndio watakuwa wakipeleka maziwa kwenye kiwanda hicho kitakapo kamilika.