Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimwelezea namna taasisi hiyo inavyofanya kazi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi alipofanya ziara katika taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akimjulia hali mtoto aliyelazwa katika wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jana kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo .
Daktari bingwa wa wagonjwa waliolazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Vivian Mlawi akimwelezea Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi namna ambavyo wanatoa huduma ya uangalizi maalum kwa watoto waliolazwa katika chumba hicho wakati alipofanya ziara ya kutembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kuangalia huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Afisa muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Mzunga akimwelezea Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi huduma wanazozitoa kwa watoto wanaotibiwa kwenye kliniki ya watoto wenye matatizo ya moyo alipofanya ziara jana ya kutembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa .
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akiangalia maktaba ya watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake ya kutembelea taasisi hiyo kwa ajili kuangalia huduma zinavyotolewa.
Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Raymond Machari akimuonesha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi ujumbe ufupi wa simu kutoka kwa wananchi wanaopatiwa huduma kupitia namba maalum ya kufikisha maoni ya wananchi wakati wa ziara yake aliyoifanya katika taasisi hiyo kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa .
Afisa muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anayefanya kazi katika mtambo wa Cathlab Rydiness Mulashani akimwelezea huduma za uchunguzi, upasuaji mdogo wa moyo pamoja na upandikizaji wa vifaa visaidizi vya moyo zinazotolewa katika chumba hicho Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi alipofanya ziara katika taasisi hiyo kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa.
Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Daniel Bunare akimwelezea Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi namna ambavyo mfumo wa manunuzi unavyotumiwa na taasisi hiyo katika manunuzi mbalimbali wakati wa ziara yake ya kutembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akielezea mafanikio ya taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi aliyoifanya katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na watendaji wa hiyo mara baada ya kumaliza ziara yake ya i kuangalia huduma zinazotolewa na JKCI jana Jijini Dar es Salaam kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi.
Picha na: JKCI
………………………………………………………………….
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Kuwepo kwa maktaba za watoto katika Hospitali kunawajenga kiakili siyo kwamba wanakwenda kupata matibabu peke yake bali pia wanapata elimu ya darasani kwa muda wanaopata au kusubiri tiba.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi alipofanya ziara ya kutembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na kuwakuta watoto wakiwa katika maktaba wanajisomea.
Dkt. Yonazi alisema hakuwahi kufikiria kwamba hospitali inaweza kuwa na maktaba ambayo itawawezesha wagonjwa wakiwemo watoto kusoma vitabu wakati wakisubiri kupata matibabu au wakiendelea na matibabu yao.
“Ni muhimu mtoto akapata elimu, Hospitali ikitoa kipaumbele kwa watoto wanaokaa muda mrefu wakipata matibabu wakapata elimu kwa kuwajengea maktaba itawasaidia kuwajenga kiakili pamoja na kuwa wanaumwa lakini pia wanapata haki yao ya msingi ya kupata elimu sawa na watoto wengine”,.
Dkt. Yonazi alisema kuwepo kwa maktaba hiyo kumemshangaza na kupata jibu kuwa watoto wanatakiwa kupata elimu wakiwa hospitali wakati wanaendelea kupata huduma za matibabu.
Naibu Katibu Mkuu huyo pia aliwapongeza wafanyakazi wa Taasisi hiyo kwa huduma ya matibabu ya moyo wanayoitoa kwa wagonjwa na kusema kuwa kwa kufanya hivyo wagonjwa wanafarijika kutokana na huduma wanayoipata.
“Kila eneo nililopita nimeona wafanyakazi wanawahudumia wagonjwa kwa kujituma na wanaonesha sura za kutabasamu hakika huduma hii mnayoitoa ni faraja kubwa kwa wagonjwa na watu wengine wanaokuja katika Taasisi hii kupata huduma”, alipongeza Dkt. Yonazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutembelea Taasisi hiyo na kusema kuwa wamefarijika kuona kiongozi wa Serikali amewatembelea na kuwaomba viongozi wengine watembelee Taasisi hiyo ili waone huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Prof. Janabi alisema changamoto kubwa iliyopo ni hakuna data base ya kupata idadi sahihi ya wagonjwa wa moyo hapa nchini jambo ambalo linawafanya washindwe kutunza kumbukumbu lakini kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo kumbukumbu zao wanazo na inawasaidia kuwafuatilia wagonjwa hao.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha katika watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai mmoja ana tatizo la moyo.
Kwa Tanzania takwimu zinaonesha kila mwaka watoto wanaozaliwa wakiwa hai ni milioni mbili na wenye matatizo ya moyo wanakadiriwa kuwa zaidi ya elfu 13 lakini haijulikani ni watoto wangapi wanazaliwa wakiwa na matatizo ya moyo na wangapi watahitaji kutibiwa na kwa wakati gani.
“Katika Taasisi yetu tuna kipimo cha kuangalia mtoto aliyepo tumboni kama ana matatizo ya moyo au la (Fetal echocardiography). Kwa kufahamu tatizo tunamshauri mama mjamzito ni hospitali gani aende kujifungua pia inatusaidia kumfuatilia mtoto ili pindi atakapozaliwa aanze matibabu ya moyo mapema”,.
“Mama mjamzito naye akiwa na tatizo la moyo ukimwambia ajifungue kwa njia ya kawaida anaweza kupoteza maisha lakini kama mama huyu atagundulika kuwa na tatizo la moyo atashauriwa ajifungue kwa njia ya upasuaji ili awe salama yeye na mtoto wake aliyepo tumboni”, alisema Prof. Janabi.