Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanal Ngemela Lubinga akiongea na wananchi wilayani Urambo Mkoani Tabora wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mkoani humo.
…………………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewahakikishia wakazi wa wilaya ya Urambo na Kaliua Mkoani Tabora kuwa kero ya kukatika katika umeme katika wilaya hizo itamalizika hivi karibuni baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha kupozea umeme kinachojengwa katika kijiji cha Uhuru kata ya Vumilia wilayani Urambo.
Hayo yamebainishwa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM anayeshughulikia Siasa na Mahusiano ya Kimataifa Kanali Ngemelela Lubinga alipokuwa akiongea na wakazi wa vijiji vya Msengesi na Izimbili vilivyoko katika kata ya Uyumbu.
Alisema kuwa mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Umeme nchini umekusudia kuongeza nguvu ya nishati hiyo katika wilaya hizo 2 na kumaliza kero ya kukatika mara kwa mara kwa umeme huo.
Alisisitiza kuwa kazi ya ujenzi wa mradi huo inaendelea, hivyo akawataka wakazi wa wilaya hizo kuendelea kuamini serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi kuwa ina dhamira ya dhati ya kumaliza kero hiyo.
‘Nimewasiliana na Waziri wa Nishati Januari Makamba, amenihakikishia kuwa fedha za kutekelea mradi huo zipo na kazi ya utekelezaji mradi huo inatarajiwa kukamilika mapema kabla ya mwezi Machi mwakani’, alisema.
Awali baadhi ya wananchi walimweleza Lubinga kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na kero kubwa ya maji na umeme kukatika mara kwa mara jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo yao kiuchumi, hivyo wakaomba awafikishie kilio hicho serikalini.
Kanal Lubinga alibainisha kuwa ujio wa mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Viktoria ambao sasa umeshafika mjini Tabora ni suluhisho la maji katika wilaya zote za Mkoa huo, alishauri fedha zozote zinazoletwa kwa ajili ya miradi mingine ya maji ziongezwe katika mradi huo mkubwa ili maji yafike haraka.
Alisisitiza kuwa katika hili watamshauri Waziri wa Maji Jumaa Aweso kutumia mbinu hiyo ili kuharakisha maji katika wilaya zisizokuwa na huduma na maji safi na salama.
Aidha alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha fedha zote zaidi ya bil 2 zilizoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, afya na barabara zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa.