Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Pangani Magharibi, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.
Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Pangani Magharibi, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akielekea kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF kwa baadhi ya walengwa wanaonufaika na miradi hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani jijini Tanga.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Mtaa wa Majengo Kuu, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Bibi Fatuma Salim wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Ndejembi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.
………………………………………………………..
Na. Veronica Mwafisi-Pangani
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amefurahishwa na matumizi mazuri ya ruzuku kwa baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani jijini Tanga.
Akizungumza na walengwa wa Mpango huo katika Kijiji cha Pangani Magharibi, Mhe. Ndejembi amesema amefarijika kuona kaya tatu alizozitembelea ambazo hapo awali zilikuwa zikiishi katika mazingira magumu lakini hivi zinaishi maisha mazuri kwa sababu zimeweza kutumia vizuri ruzuku ya TASAF wanayoipata.
“Nimeshuhudia baadhi ya walengwa hawa kuwa wabunifu wa kutengeneza bidhaa mbalimbali na kuziuza ili kujiongezea kipato,” Mhe. Ndejembi amesema na kuongeza kuwa walengwa hawa wanapata ruzuku sawa na wengine lakini wao wamejiwekea malengo yenye tija hivyo kila mlengwa ni vizuri akawa na malengo kama hayo.
Mhe. Ndejembi amesema, Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ina miradi mingi sana ya kutekeleza lakini badala ya kuelekeza fedha zote kwenye miradi hiyo iliona ni vizuri izielekeze pia kwenye kaya maskini ili kaya hizo ziweze kuboresha maisha yao, hivyo ni vema wakazitumia vizuri ili kumuunga mkono kwa kutekeleza kaulimbiu ya Kazi Iendelee kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu ili kufikia malengo.
Amewataka walengwa wapya walioandikishwa hivi karibuni kuhakikisha wanaweka malengo ya ruzuku watakayoipata kuhakikisha wanatumia ruzuku hiyo kwa kujiendeleza kimaisha na kuinua uchumi wao badala ya kutumia kwenye anasa.
“Niwaombe sana kuanzia sasa muanze kutumia fedha hizi vizuri, mzipangie bajeti vizuri, muweke malengo mazuri ya kuwa na maisha bora ikiwemo kula vizuri, kujenga nyumba na masuala mengine ya maendeleo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi yuko Jijini Tanga kwenye ziara ya kikazi ya siku tatu ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF ambapo ameanza na Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.