Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua mafunzo kwa Watendaji wa kata na vijiji yanayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Taasisi ya Hanns Zaidel Foundation kwenye ukumbi wa Narungombe, Ruangwa,
Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa watendaji wa kata na vijiji yanayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Taasisi ya Hanns Zaidel Foundation wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua mafunzo hayo kwenye ukumbi wa Narungombe, Ruangwa, Novemba 22, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Askari Kata wafanye kazi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya utumishi waona waache tabia za ubabe na vitisho kwani zitaleta mpasuko kati yao na wananchi na hatimaye watashindwa kutekeleza majukumu yao.
Pia, Waziri Mkuu amewataka Watendaji wote wa Kata, Vijiji, Mtaa na Vitongoji waimarishe mifumo ya udhibiti kwa kuanzisha na kutumia daftari lenye orodha ya wakazi. “Wekezi mifumo ya kujua nani ameingia na lini atatoka kwenye mitaa yenu ili kubaini viashiria vyote vya usalama.”
Ametoa msisitizo huo leo (Jumatatu, Novemba 22, 2021) wakati akifungua Mafunzo ya Watendaji wa Kata na Vijiji yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi Tanzania na Taasisi ya Hanns Seidel Foundation (HSF), Ruangwa mkoani Lindi.
Waziri Mkuu amesema askari hao wasipofanya kazi kwa kuzingatia maadili watashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, amewasisitiza waimarishe uhusiano mwema wa kikazi na wananchi wanaowatumikia na wasiwe chanzo cha uvunjifu wa amani.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi wawapokee Askari Kata katika maeneo yao na kwamba hao si adui zao bali ni marafiki ambao wanawahitaji katika kutenda kazi zao, hivyo wawape ushirikiano mkubwa katika masuala yote ya ulinzi na usalama.
Amesema Serikali imeridhia mafunzo hayo yafanyike kwa kujua umuhimu wake kwao, hivyo ni anatarajia watayapa umuhimu mkubwa kama inavyotakiwa. “Utaratibu uwekwe ili watendaji wa ngazi ya kata za vijiji katika kila halmashauri nchini wapate mafunzo haya.”
Waziri Mkuu amesema kuwa ana imani kupitia mafunzo hayo watendaji hao watapata ujuzi na maarifa ambayo yatawajengea fikra chanya kuhusu suala la ulinzi na usalama na hatimaye watakuwa wazuri zaidi
“Na matarajio ya Serikali ni kwamba mtaenda kufanyakazi kwa kuzingatia yote mtakayoyapata kutokana na mafunzo haya. Mafunzo haya yatawawezesha kutekeleza kikamilifu majukumu mahsusi ikiwemo kuwezesha na kudumisha utulivu, amani na utawala bora.”
Pia Waziri Mkuu amesema baada ya mafunzo hayo watendaji hao wanapaswa kuwa kiungo bora na Jeshi la Polisi ili waendelee kudumisha uhusiano mwema baina yao na wananchi wanaowatumikia.
“Uhusiano mwema utawafanya wananchi wawaamini na wawe huru kuwapa ushirikiano wote mnaohitaji katika kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yenu ya utendaji. Kaimarisheni uhusiano wa wananchi na Jeshi la Polisi ili tuweze kufanikiwa kuwa na jamii yenye imani na Jeshi letu, hivyo kuwa na utayari katika kushiri kulinda amani na usalama wa watu na mali zao”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa wadau wote wa masuala ya ulinzi na usalama kwa pamoja washirikiane katika kujenga mazingira mazuri ya wananchi kushiriki katika kujilinda wenyewe pamoja na mali zao.
“Pamoja na hilo pia toeni ushirikiano mkubwa kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na hatimaye kuendelea kudumisha azma ya Serikali yetu ya kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kisiwa cha amani”
Naye, Kamishina wa Ushirikishwaji wa Jamii kutoka Jeshi la Polisi, Dkt Mussa Ali Mussa amesema utekelezaji wa mradi huo wa Polisi Kata ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi yenye lengo la kuhakikisha wanaweka uhusiano wa karibu wa kiutendaji kati ya Polisi, Watendaji wa kata pamoja na Madiwani.
Awali, Mkurugenzi Mkazi wa taasisi ya Hanns Seidel Foundation Tanzania na Uganda Karl Peter Schoenfisch amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwafanya wananchi kutambua wajibu wao katika jamii zao na kuweza kutoa ushirikiano kwa Askari Kata kila inapohitaji, hivyo kupunguza uhalifu katika maeneo yao.