NA BALTAZAR MASHAKA,Ilemela
SERIKALI mkoani Mwanza imewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuhakikisha wanadhibiti matumizi yasiyo sahihi ya fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa yakamilike kwa viwango na thamani ya fedha ionekane.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhandisi.Robert Gabriel wakati akikagua miradi ya maendeleo ya elimu inayotekelezwa mkoani humu kwa fedha za serikali zilizotolewa kukabiliana na ugonjwa wa Uviko-19.
“Kwa fedha alizotoa Rais Samia Suluhu Hassan,kutokana na viashiria vya ubadhirifu kwenye miradi ya aina hii,tuendelee kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya fedha hizo kupitia taarifa za kamati za ujenzi ili miradi ikidhi viwango vya ubora,thamani ya ionekane,chenchi ibaki na itumike kutatua changamoto kwenye maeneo mengine na kuleta tija,”alisema
Alisema kupitia miradi yote ya madarasa 985 yanayojengwa mkoani humu,amejiridhisha baada ya kukagua na kuangalia hatua ya ujenzi wa miradi hiyo ilikofikia na fedha iliyotumika, mwelekeo ni mzuri na kusistiza,ikikamilika samani (viti na meza)nazo ziwe tayari,pia watumie tarazo au sakafu ya kawaida badala ya vigae.
Aidha alipongeza uongozi kwa usimamizi wa miradi hiyo na ubunifu wenye tija uliotumika kuleta vifaa eneo la miradi,umeonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kutanguliza taifa mbele,hivyo fedha zitakazobaki waangalie maeneo yenye mapungufu na kushauri mtindo huo utumike maeneo mengine ili kutumia fedha kwa umakini.
“Niwapongeze Ilemela katika mkoa mzima kwa taarifa nilizo nazo mnaongoza kwa kasi kubwa kwenye miradi hii,wapo walio zaidi ya asilimia 70 kwenye upande wa hatua za maboma kwenda juu,wengine kidogo wapo hatua za chini lakini nao nitawatembelea ili kujiridhisha na kuweka hamasa ili kuweza kufikia lengo,” alieleza Mhandisi.Gabriel.
Mkuu wa shule ya sekondari Kilimani Majaliwa Gerana alisema shule hiyo ilipokea milioni 40 za vyumba viwili vya madarasa pamoja na seti 100 ya viti na meza ambapo ujenzi umefikia asilimia 70 na kasi inaendelea kwa kuzingatia ubora na viwango elekezi.
“Mradi huo utakapokamilika utapunguza uhaba wa vyumba vya madarasa kutoka vyumba sita na kubaki vyumba vinne pia utapunguza upungufu wa meza kutoka 216 hadi kufikia 116,tunaomba utuombee shule iingie kwenye mpango wa bweni,”alisema Gerana.
Mkuu wa shule ya Sekondari Buswelu, Arsen Peter,akitoa taarifa ya ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa katika shule hiyo alieleza kuwa ujenzi utagharimu zaidi ya milioni 99.9 kati ya hizo,fedha za serikali kuu ni milioni 100, nguvu za wananchi sh.milioni 8.
Alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaboresha mazingira ya kufundishia, kujifunza, kupunguza mrundikano wa wanafunzi darasani,kuongeza molari ya wanafunzi kujifunza kwa bidii pamoja na kuongeza molari ya walimu kufundisha.
Naye Mkuu wa sekondari ya Bujingwa, Oliver Kimathi alieleza shule ilipokea sh. milioni 80 za vyumba vinne vya madarasa ikiwa ni jitihada za serikali kuondoa tatizo la mrundikano wa wanafunzi darasani na kukabiliana na janga la UVIKO-19.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela, Mhandisi.Modest Apolinnary,alisema wanakaribia asilimia 50 ya utekelezaji wa miradi yote na ina kwenda vizuri,matarajio ni kuikamilisha kabla ya Desemba 15 mwaka huu na kuzipongeza kamati za usimamizi za ujenzi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Massala, alisema wanaendelea kusimamia fedha iliyotokewa katika manispaa hiyo kadri ya maelekezo yalivyotolewa na kuishukuru serikali kuwapatia fedha sh. bilioni 1.84 za kujenga vyumba 97 na wanatarajia kukabidhi vyote vikiwa vimekamilika.
Miongoni mwa shule alizotembelea Mhandisi.Gabriel kukagua ujenzi wa madasara ni Buswelu,Bujingwa na Kilimani na kueleza mkoa ulipokea fedha za kujenga madarasa 985 hivyo ameanza ufuatiliaji kuona zinavyofanya kazi.