******************************
Na Mwandishi wetu, Hanang’
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, wamejengewa uwezo kwa kupatiwa elimu ya ufugaji wa kisasa wa samaki kwa njia ya vizimba kwa manufaa ya wavuvi wao.
Mkurugenzi wa kampuni ya KCG Aquatec fish farming consultancy, Stephano Karoza ametoa mafunzo hayo kwenye baraza la madiwani wa halamshauri hiyo alipoalikwa Kwa ajili ya kutoa somo hilo.
Karoza amesema teknolojia ya sasa ya ufugaji inahitaji vizimba kutokana na upungufu wa maji na mazingira ya watanzania wengi siyo rafiki katika kufanya shughuli za uvuvi wa kawaida.
Amesema shughuli za uvuvi wa kisasa wa vizimba unaweza kufanywa kwa kufuga baharini, ziwani, kwenye mto au malambo hivyo wavuvi wachangamkie fursa hiyo.
Amesema serikali imekuwa ikihamasisha uvuvi wa vizimba kwani ufugaji uliozoeleka una changamoto nyingi ila awali sheria za mazingira zilikuwa hazijaruhusu uvuvi huo.
“Wenzetu Kenya na Uganda wameshaanza kufuga kwa kutumia teknolojia hiyo na miaka minne iliyopita serikali yetu ilitoa ruhusa ya uvuvi wa vizimba kwenye bahari na maziwa,” amesema Karoza.
Amesema hivi sasa kwenye ziwa Victoria, Serikali, wajasiriamali kupitia vikundi wamegeukia uvuvi huo na wapetoa kipaumbele katika kujihusisha na shughuli za uvuvi wa kutumia vizimba.
Amesema matumizi ya samaki yanazidi kuongezeka kila kukicha hivyo wavuvi wanapaswa kubadilika kwa kugeukia uvuvi wa samaki wa njia ya vizimba ili kuvua kwa tija zaidi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya wilaya ya Hanang’ Rose Kamili amesema hiyo ni fursa nzuri kwa wananchi wa Kata yake ya Bassotu ambao ni wavuvi wa bwawa la Bassotu.
“Inabidi mfike hadi kwenye kata yangu ya Bassotu mkawafundishe zaidi wananchi wetu waweze kuvua samaki kwa njia bora zaidi na yenye tija,” amesema Kamili.