Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akizungumza na wananchi wake wa Tarafa ya Mlimba
Wananchi wa Tarafa ya Mlimba Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo hilo, Godwin Kunambi alipofika kuzungumza nao ambapo ameeleza mafanikio yake ndani ya kipindi cha miezi 11.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akigawa vocha kwa kikundi Cha akina Mama ambapo wamepatiwa mkopo wa Sh Milioni Nane na Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi ( wa pili kutoka kuahoto) akiwa amebeba bomba la Maji Pamoja na wananchi wake wakati gari lililobeba mabomba yenye thamani ya Sh Milioni 370 yalipofika katika eneo la Udagaji.
………………………………………………………………………
MBUNGE wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro, Godwin Kunambi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua hatua za kumaliza changamoto ya maji katika Tarafa ya Mlimba Jimboni humo baada ya kutoa kiasi cha Sh Bilioni 3.6 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji utakaohudumia zaidi ya Kata nne na vijiji 11 vya Tarafa hiyo.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wananchi wa Tarafa hiyo ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kitarafa ya kueleza mafanikio yake ndani ya miezi 11 tokea aapishwe kuwa Mbunge sambamba na kugawa hundi yenye thamani ya Sh Milioni 918 kwa vikundi 100 katika Tarafa za Mlimba na Mngeta.
Akizungumza na wananchi hao wa Mlimba, Kunambi amesema kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na Rais Samia tayari kimeshafika sambamba na kuletewa mabomba ya maji katika eneo la Udagaji ambayo yana thamani ya Sh Milioni 370.
“Kwa dhati nimshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa sababu amesikia kilio chetu wananchi wa Mlimba na kutupatia fedha nyingi Sh Bilioni 3.6 kwa ajili ya mradi mkubwa wa Maji ambao utamaliza changamoto hii ya muda mrefu katika vijiji 11 vilivyopo katika Kata za Chisano, Karogakendo, Kamwene, Ching’anda na hapa Mlimba.
Mradi huu wa Maji utatekelezwa kwa miaka Mitano na itakapofika 2025 habari ya Maji haitoongelewa tena hapa Mlimba, haya yote ni mapenzi ya Rais wetu kwa wananchi wa Mlimba,” Amesema Kunambi.
Akizungumzia miundombinu ya Barabara, Kunambi pia amemshukuru Rais Samia kwa kumpatia kiasi cha Sh Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ambapo Kata ya Mlimba pekee itapata takribani Sh Milioni 500.
” Kuna Kila sababu ya kumshukuru Rais Samia alitoa Sh Milioni 500 kwa ajili ya Barabara za TARURA Kwa Wabunge wote lakini Sisi Mlimba akatuongezea fedha zingine na hivyo tukapata Bilioni 1.5. Hapa Kata ya Mlimba pekee tumeleta Sh Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Carlifonia, Makete, Tazara na Mwangoma, lengo letu ni Mlimba iwe na hadhi kama Mji Mdogo,” Amesema Kunambi.
Mbunge Kunambi pia amesema kupitia fedha za Uviko-19 ambazo Serikali imepatiwa na IMF tayari Jimbo la Mlimba limepatiwa kiasi Cha Sh Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Madarasa takribani 80 jambo ambalo litaondoa michango ya wazazi Januari mwakani Shule zitakapofunguliwa.