Sehemu ya mji wa manispaa ya Mpanda
Moja ya Choo katika manispaa ya mpanda
***************************
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Wanafunzi wa shule za msingi katika mkoa wa Katavi bado wanakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo ambapo mkoa mzima una jumla ya wanafunzi 226,041 wa shule za msingi wakati matundu ya vyoo ni 2978 katika shule mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Afisa Elimu taaluma mkoa wa Katavi Florence Ngua amesema kati ya wanafunzi hao wanafunzi wa darasa la awali wapo 18,241 ambao nao wanalazimika kukabiliana na changamoto hiyo.
Bwana Ngua alieleza kuwa kufuatia upungufu huo mkoa unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa matundu ya vyoo ambapo hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu Zaidi ya matundu 1,000 ya vyoo yanaendelea kujengwa.
“Haya matundu mapya yakikamilika yatapunguza msongamano wa wanafunzi vyooni kwa kiasi kikubwa” alisema Ngua
Akizungumzia hali ya vyoo katika manispaa ya Mpanda Afisa Afya wa manispaa ya Mpanda Erick Kisaka ameeleza kuwa wakazi wa Manispaa walio wengi wana vyoo vya kisasa.
Kwa manispaa ya Mpanda asilimia 86.2 ya kaya 31,000 zinatumia vyoo bora na asilimia 13.7 wanatumia vyoo visivyo bora na asilimia 0.1 sawa na kaya 30 hawana vyoo kabisa.
Aidha aliongeza kuwa kuhusu unawaji wa mikono ambao unakwenda sambamba na matumizi ya vyoo hali bado sio nzuri sana.
Kuhusu uwiano wa matumizi ya vyoo mashuleni ameeleza kuwa bado Manispaa haijatimiza uwiano unaotakiwa ambapo inatakiwa tundu moja la choo litumiwe na wavulana hamsini wakati kwa wasichana arobaini linatakiwa kutumika tundu moja la choo.
Afisa Afya huyo pia amewashauri wanaoendesha shule za awali kuwawekea watoto wadogo wa umri wa miaka mitatu hadi minne vyombo maalum vya kujisitiri (Poti) ili kuwaepusha na madhara yanayoweza kujitokeza kwa kutumia vyoo kwa kuchangia na watoto wakubwa.
Leo dunia imedhimisha siku ya choo duniani, ambapo takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba watu bilioni 3.6 bado wanakosa huduma hiyo muhimu ya kujisitiri na usafi ndio maana maudhui ya mwaka huu ikieleza “kuthamini vyoo” lengo likiwa kuichagiza dunia na wadau wote kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa kila mtu kila mahali.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi wakizungumzia cchangamoto hiyo wamesema upungufu wa vyoo pia unachangia usafi kuwa duni katika vyoo vya shule.
“Kwakweli ni changamoto kila mara watoto wanaugua U.T.I ni hospitali kila siku” alisema Rehema Chamgoni mkazi wa Manispaa ya Mpanda mzazi wa mtoto darasa la kwanza shule ya msingi Kashato.