Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto), akimsikiliza kwa makini Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Nicodemus Mkama, alipokuwa akieleza utekelezaji wa bajeti ya Mamlaka hiyo kwa mwaka wa Fedha 2018/19, jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, akitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), kuhakikisha inaorodhesha Kampuni nyingi katika Soko hilo ili kuweka uwazi zaidi katika utendaji wao na kuchangia katika ongezeko la mapato ya Serikali kwa njia ya kodi.
Mkutano kati ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (mbele) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Nicodemus Mkama (wa pili kulia), ukiendelea katika ofisi za CMSA jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (wa pili kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Nicodemus Mkama (wa tatu kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa waandamizi kutoka CMSA na Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kumaliza Ziara ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 wa CMSA, jijini Dar es salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Nicodemus Mkama, wakipeana mkono baada ya kumaliza Ziara ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 ya CMSA, jijini Dar es salaam.
(Picha na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam)
…………………….
Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imeitaka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kuhakikisha Kampuni nyingi zinaorodheshwa katika Soko la hisa ili kuweka uwazi zaidi katika utendaji wa kampuni hizo na hivyo kuwezesha Serikali kukusanya kodi stahiki na kuchangia katika ongezeko la mapato ya Serikali.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alipofanya ziara katika Mamlaka hiyo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 katika Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Dkt. Kazungu, alisema kuwa CMSA iendelee kusimamia masoko ya Mitaji ya Dhamana kwa kuorodhesha Kampuni nyingi zaidi katika soko hilo la hisa kwa kuzingatia masharti ya kuorodheshwa kampuni ili kuongeza uwazi, utawala bora na ufanisi wa kampuni hizo kwa kuweka mazingira mazuri ya uendeshaji na uwazi wa hesabu zao, hatua itakayochangia kukuza uwekezaji na mapato ya Serikali hususani katika eneo la kodi.
“Muendelee na kasi ya kutoa elimu kwa wananchi wengi ili waweze kujiunga na Masoko ya Hisa hususani kwa wananchi walio katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”, alieleza Dkt. Kazungu.
Alisema kuwa iwapo wananchi wengi watajiunga katika Masoko la Hisa kutawafanya kuongeza mapato yao lakini pia kushiriki katika umiliki wa uchumi wa nchi yao.
Dkt. Kazungu alisema kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa uchumi wa viwanda, uchumi unaotarajiwa kujengwa katika kipindi kifupi wakati wa kuelekea katika uchumi wa kati hivyo ni vema wawekezaji wakahimizwa kupata mitaji ya kuendeleza na kupanua uwekezaji kupitia masoko ya mitaji na kutoa fursa nyingi za uwekezaji kwa wananchi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Nicodemus Mkama, amesema Mamlaka yake imeweka mkakati wa kutoa elimu kwa umma na wawekezaji mbalimbali jinsi ya kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.
“CMSA inaendelea kutoa elimu kwa umma na kwa makundi mbali mbali ya wanataaluma, wanafunzi wa elimu ya juu, watunga sera ikijumuisha Kamati za Bunge. Elimu hii inalenga kuelimisha umuhimu na fursa ya masoko ya mitaji katika kukuza uchumi na ushirikishwaji wa wananchi katika Sekta ya Fedha hususani masoko ya mitaji” alifafanua Bw. Mkama.
Alisema kutokana na jitihada hizo, kwa sasa uhitaji katika uwekezaji katika Soko ni mkubwa, hii inawafanya kuongeza bidhaa zinazokidhi matakwa ya wawekezaji ndani na nje ya nchi.
“Hii imejidhihirisha hivi karibuni kwa kuongezeka kwa kampuni nyingi katika sekta ya fedha kuorodhesha hatifungani ikiwa ni njia sahihi ya taasisi hizo kupata fedha za mahitaji mbalimbali ya utoaji mikopo na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Alisema elimu hiyo pia imeleta matokeo chanya na mwitikio wa matoleo ya hatifungani za Kampuni ya Kuendeleza Sekta ya Nyumba – TMRC, Benki ya Biashara ya DCB na Benki ya Biashara ya NMB na unaonyesha wazi kuwa kuna ongezeko kubwa la uelewa wa wananchi kushiriki katika uwekezaji kwenye masoko ya mitaji.
Toleo la hatifungani ya NMB Bank limeweka historia kubwa katika maendeleo ya masoko ya mitaji hapa nchini kwa kupata kiwango cha shilingi bilioni 83.3, ikiwa ni mafanikio ya asilimia 333 ikilinganishwa na shilingi bilioni 25 zilizotarajiwa kukusanywa.
Bw. Mkama alisema kuwa mauzo hayo yamekuwa na idadi na thamani kubwa kuliko mauzo yote ya hatifungani yaliyowahi kufanyika hapa nchini, ambapo jumla ya wawekezaji 2,264 wameweza kushiriki. Kati ya wawekezaji hao, asilimia 99.5 ni wawekezaji wadogo wadogo, na wawekezaji Kampuni ni asilimia 0.5.
“Tumeshatoa maelekezo kwa watendaji na washiriki (wanaotoa dhamana) katika Masoko ya Mitaji kuhakikisha wanakuja na bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wawekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi watakao sababisha ongezeko la mapato yao na upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo jambo litakalochangia kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi”, alieleza Bw. Mkama.
Alisema kuwa katika utoaji wa elimu, CMSA inatumia mbinu mbalimbali za kibunifu ikiwa ni pamoja na kuweka mashindano kwenye Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania Bara na Visiwani kwa kuwezesha wanafunzi kujifunza elimu ya masoko ya mitaji kwa njia ya kujibu maswali na kuandika insha
Alibainisha kuwa, wanafunzi wanaofanikiwa kushinda nafasi ya kwanza hadi ya tatu wanapewa tuzo mbalimbali zikiwemo fedha taslimu kuanzia shilingi milioni moja hadi milioni 1.8 kama kivutio cha ushiriki huku wanafunzi walioshika nafasi 20 za juu wanazawadiwa shilingi laki 2 kila mmoja na kwamba washindi wa nafasi ya kwanza hadi ya tatu wa mwaka huu (2019) watapelekwa nchini Namibia kwa ziara ya mafunzo.