……………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Mafia
WAKALA Wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA ) ,imepokea gawio la kiasi cha sh .Bilioni 78 kutoka katika fedha za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko19 ambapo kati ya fedha hiyo mkoa wa Pwani utapata miradi 8 yenye thamani ya Bilioni 3.7.
Akielezea kuhusu fedha hiyo waliyopokea kutoka serikalini , baada ya kutembelea miradi ya maji na visima Mafia, Mkurugenzi Mkuu RUWASA, Clement Kivegalo alisema ,fedha hiyo ni nyingi hivyo wataisimamia na kutekeleza miradi lengwa kwa wakati.
Kivegalo alieleza ,agizo lililopo ni kila mradi usizidi sh.milioni 500 ,kwa mkoa wa Pwani imepata Bilioni 3.7 kati ya Bilioni 78 ambayo imegawanywa pia kwenye mikoa mingine kwa ajili ya miradi iliyo chini ya RUWASA.
Nae Meneja RUWASA Pwani, Beatrice Kasimbazi alisema, asilimia 76 ya watu wanapata maji Mkoani humo , ikiwemo mjini wanapata maji kwa asilimia 84 na Vijijini asilimia 72.
Alieleza ,bajeti ya mwaka huu wametengewa kiasi cha sh.Bilioni 21 ambapo Bilioni 3.7 Ni kutoka katika fedha za Uviko19, Bilioni 15 kutoka mfuko wa maji huku fedha iliyosalia Bilioni 2.9 ni kwa ajili ya miradi ya PBR.
“Hapo tutatekeleza miradi Kama 30 Lakini katika gawio la fedha ya Uviko19 itatekeleza miradi 8 ,Tunashukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji Vijijini, :;”Huu ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kufikisha maji Vijijini na mjini,:”
“Tutahakikisha Shule , Zahanati ,masoko ,na sehemu za mikusanyiko inapata maji ili kuhakikisha maeneo ya mkusanyiko,wananchi wananawa maji tiririka kama wataalamu wanavyoshauri na kupambana na ugonjwa wa Uviko19.”alifafanua Kasimbazi.
Kasimbazi alisema ,agizo lililopo ni kuhakikisha ikifika March 2022 miradi hiyo iwe imekamilika na itoe huduma ,hivyo basi amejipanga na mameneja wa wilaya na watendaji wake kutekeleza agizo hilo kwa vitendo.
Mkuu wa wilaya ya Mafia, Mhandisi Martin Ntemo, aliishukuru RUWASA kwenda kutembelea miradi na visima vinne wanavyochimba mwaka huu ndani ya vijiji ambavyo wanategemea kuongezwa kufikia visima 10.
Aliwaelekeza viongozi wa vijiji na wananchi kulinda miundombinu na vyanzo vya maji .
Ntemo alisema, watakaoenda kinyume na hilo kwa kuchoma Moto,kufuga mifugo , ama kufanya shughuli za kijamii ,katika vyanzo vya maji watachukuliwa hatua za kisheria.
Meneja wa RUWASA Mafia Clement Lyoto,alibainisha kwa mwaka huu wametenga milioni 50 kwa ajili ya kutafuta vyanzo vya maji vinne .