Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Nchi ya Singapore, mazungumzo yaliolenga kuimarisha ushirikiano pamoja na uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini Tanzania. Mazungumzo hayo hayo yamefanyika katika eneo la Shangri La, nchini Singapore.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Nchi ya Singapore, mazungumzo yaliolenga kuimarisha ushirikiano pamoja na uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini Tanzania. Mazungumzo hayo hayo yamefanyika katika eneo la Shangri La, nchini Singapore.
………………………………………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Wafanyabiashara na wawekezaji wa Nchi ya Singapore, mazungumzo yaliofanyika katika hoteli ya Shangri La nchini Singapore.
Wafanyabiashara hao wamemueleza Makamu wa Rais nia yao ya kuwekeza nchini Tanzania na kuiomba serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kuondoa vikwazo hasa katika masuala ya biashara ya kilimo, kuongeza ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na kuomba kuendelea kuimarika kwa ushirikiano baina ya Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kurahisisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa zitakazozalishwa.
Akizungumza na wafanyabishara hao Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametaja hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuweka mazingira salama ya uwekezaji ikiwemo kuendeleza miradi mikubwa itakayotoa unafuu katika kuwekeza kama vile Ujenzi wa mradi wa Umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (JNHPP), Ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR),Kuboresha shirika la ndege ambapo mpaka sasa jumla ya ndege 11 zimekwisha nunuliwa,kuboresha bandari, kuwekeza katika kutoa nishati vijijini, kuboresha miundombinu pamoja na huduma za kijamii.
Amesema serikali imeendelea kuweka mkazo katika uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa kutunga sera na kufanya marekebisho ya sheria zinazorahisha ufanyaji biashara pamoja na kutatua changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara kupitia Baraza la Biashara la Taifa ambalo huongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji kutoka Singapore kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za viwanda hasa viwanda vya dawa na vifaa vya umeme, kuwekeza na kuweka ushirikiano katika sekta ya bandari hasa katika miundombinu ya bandari,usafiri pamoja na mifumo ya Tehama. Aidha Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji hao katika sekta ya utalii kuwekeza katika miundombinu yake ikiwemo hoteli na kumbi za mikutano. Ameongeza kwamba wawekezaji hao wanaweza kushirikiana na Tanzania katika kutoa mafunzo hasa katika vyuo vya ufundi pamoja na sekta ya afya.
Amesema mkoa wa Dodoma ambao ndio makao makuu ya nchi na serikali umekuwa na maeneo mengi ya uwekezaji kutokana na kuendelea kuvutia watu wengi kuishi katika mkoa huo hivyo wawekezaji hao wanaweza kuwekeza katika miundombinu mbalimbali kama vile nyumba za makazi pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya.
Makamu wa Rais amewahakikishia wawekezaji hao kwamba Tanzania itaendelea kuimarisha amani na utulivu ili kulinda biashara pamoja na uwekezaji uliofanyika kutoka ndani na nje ya nchi.