Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel (katikati) akiteta jambo na Waziri wa Afya nchini Rwanda Dkt. David Ngamije (kulia) wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Kukabiliana an Ugonjwa wa Malaria kwa Nchi za Maziwa Makuu za Afrika Mashariki uliofanyika katika Wilaya ya Kirehe Nchini Rwanda. Aliye upande wa Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbunge.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akitazama dawa
zilizotengenezwa kwa ajili ya kujikinga na mbu katika maonyesho
yaliyofanyika wakati wa Uzinduzi Mpango wa Kukabiliana an Ugonjwa wa
Malaria kwa Nchi za Maziwa Makuu za Afrika Mashariki, aliye upande wa
kulia kwake ni Waziri wa Afya wa Rwanda Dkt. David Ngamije.
Mtaalamu wa kupambana na mazalia ya mbu akiweka viuatifilu katika ndege isiyo na rubani kwa ajili ya upuliziaji wa dawa hiyo ya kuwa mazalia ya mbu, shughuli hii imefanyika wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Kukabiliana an Ugonjwa wa Malaria kwa Nchi za Maziwa Makuu za Afrika Mashariki ambapo kwa Tanzania iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Afya
Dkt. Godwin Mollel.
Mtaalam akipulizia dawa ndani ya nyumba katika kuta, hii ni afua mojawapo katika Mkakati wa kukabiliana na ugonjwa wa Malaria uliozinduliwa katika wa Mpango wa Kukabiliana an Ugonjwa wa Malaria kwa Nchi za Maziwa Makuu za Afrika Mashariki.
Ndege isiyo na rubani (drone) ikiwa angani tayari kwa ajili ya upuliziaji viuwatilifu katika shamba la mpunga eneo ambalo kuna mazalia ya mbu. Hii ni afua mojawapo ya kukabiliana na Ugonjwa wa Malaria katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Viongizi kutoka Rwanda, Tanzania, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, wakitazama ndege isiyo na rubani (drone) ambayo itatumika kwa ajili kupulizia dawa viuwatilifu kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Kukabiliana na Ugonjwa wa Malaria kwa Nchi za Maziwa Makuu za Afrika Mashariki ambapo kwa Tanzania iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel.
…………………………………………………………….
Na Englibert Kayombo – Kirehe, Rwanda
Serikali ya Tanzania imesema itashirikiana na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuhakikisha ugonjwa wa Malaria unatokomea ifikapo mwaka 2030 kwa kushirikiana pamoja katika utekelezaji wa afua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel mara baada ya kuzindua Mpango wa Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu katika kupambana na Ugonjwa wa Malaria uliofayika katika Jimbo la Kirehe nchini Rwanda.
“Mpango huu wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kushirikiana pamoja katika utekelezaji wa afua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa wa Malaria ni mzuri na utatusaidia sisi Tanzania kutimiza malengo yetu ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria ifikapo mwaka 2030” amesema Dkt. Godwin Mollel.
Dkt. Mollel amesema Tanzania itanufaika na ushirikiano huo kwa kuongezewa uzoefu wa kitaaluma kutoka kwa wataalam toka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, teknolojia mpya za kukabiliana na ugonjwa wa Malaria, udhibiti wa vimelea vya ugonjwa huo pamoja na utekelezaji wa afua za pamoja katika kupambana na Malaria.
Amesema kuwa kupitia Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na Ugonjwa wa Malaria wa Mwaka 2021 -2025, Tanzania imejipanga kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo kutoka 7.5% kwa sasa hadi kufikia 3.5% ifikapo mwaka 2025.
“Jambo hili linawezekana, tumeweza kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Malaria kwa asilimia 61 kutoka vifo 6,311 Mwaka 2015 hadi vifo 2,460 Mwaka 2020, amesema Dkt Mollel na kusitiza zaidi azma ya Serikali ni kutokomeza kabisa ugonjwa huo nchini Tanzania.
Dkt. Mollel amesema Tanzania imeweza kupiga hatua katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria kutokana na utashi wa kisiasa ulipo baina ya viongozi kwa pamoja kuwa na ajenda ya kupambana na ugonjwa wa Malaria, elimu na uhamasishaji jamii kujikinga dhidi ya mdudu mbu, kuteketeza mazalia ya mbu kwa kupulizia viuatilifu, ununuzi wa vipimo vya haraka vya upimaji ugonjwa wa Malaria (mRTD), ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya kuua mbu pamoja na upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka Serikalini na kwa wadau wa maendeleo katika utekelezaji wa afua mbali mbali za kupambana na Malaria.
Kwa upande wa Serikali ya Rwanda, Waziri wa Afya nchini humu Dkt. David Ngamije amesema kuwa ipo haja ya kuunganisha nguvu za pamoja katika kupambana na ugonjwa wa Malaria huku akitilia mkazo zaidi katika uwekezaji wa kutumia teknolojia mpya katika kudhibiti mazalia ya mbu.
Dkt. Ngamije amesema hayo kwa viongozi nchi wanachama mara baada ya kujionea mbinu za kukabiliana na mazalia ya mbu kwa kupulizia viuatilifu kwa njia ya ndege zisizo na rubani katika maeno hatarishi yenye mazalia ya mbu.