**********************************
NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
MBUNGE wa Ilemela (CCM),Dk.Angeline Mabula,amesema Watanzania wakiwemo wananchi wa jimbo na wilaya hiyo,wanatakiwa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan,kwa uamuzi wake wa busara wa kutoa fedha za ujenzi vya vyumba vya madarasa 15,000 kote nchini.
Pia amesikitishwa na baadhi ya wajumbe na viongozi wa kata na matawi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenye ilani inayotekelezwa kugoma kushiriki ujenzi huo hadi walipwe posho kinyume na miongozo ya fedha hizo kuwa wameonyesha dharau kwa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama.
Dk.Mabula alitoa kauli hiyo jana wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa madarasa 97 katika Jimbo la Ilemela na kuzitaka kamati zote za ujenzi kuendelea kushirikiana na mafundi waongeze kasi miradi ikamilike kwa wakati.
Alisema Rais Samia ametoa fedha sh.bilioni 1.84 za Uviko-19 katika Jimbo la Ilemela ili kuimarisha huduma za jamii,uamuzi ambao ni wa busara ya hali ya juu hivyo Watanzania na wananchi wa jimbo hilo wanapaswa kumpongeza.
“Rais Samia ameondoa kero na kuwapa wananchi unafuu wa michango ya kujenga madarasa, Ilemela tutunamwahidi tutazisimamia fedha hizo zilizotokana na mkopo nafuu wa mapambano ya Uviko-19 zionyeshe thamani na ubora wa majengo,yatakapokamilika mabdiliko yatonekana,”alisema Dk.Mabula.
Akikagua ujenzi wa miundombinu hiyo ya madarasa kwenye kata 10 kati ya 19 za Ilemela,alisema vyumba hivyo vya madarasa vikikamilika vitasaidia kuondoa malalamiko ya wananchi kuhusu msongamano na mrundikano wa wanafunzi,hivyo ni fursa kwa wananchi kushiriki kwa vitendo kwenye miradi hiyo badala ya malumb ano yasiyo na tija.
Mbunge huyo wa Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi,alisikitishwa na baadhi ya wajumbe wa kamati wakiwemo viongozi wa CCM Shibula kususa kushiriki ujenzi wa madarasa hadi walipwe posho,wamemgomea Mwenyekiti wa Chama Taifa na kuhoji kwa nini Kata ya Shibula ilhali maeneo mengine wamefanya,mnkwamisha juhudi za Rais Samia.
“Itakuwa ajabu, serikali inaleta fedha halafu mnagoma,mnapuuza mchango wa Rais Samia ametoa fedha watoto wasibanane madarasani, kama hatuwezi kumsaidia tunadai posho tunakwamisha juhudi zake.Rai yangu kamati za ujenzi kila kata zizingatie miongozo,kuna maeneo kasi ya ujenzi ni ndogo sababu ya malumbano,”alisema.
Dk.Mabula litumia fursa hiyo kuzipongeza kamati za ujenzi za Shule ya Sekondari Kilimani kwa kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili kwa asilimia 95 na kuzitaka kamati zingine kuongeza kasi ya ujenzi.
Meya wa Manispaa ya Ilemela na Diwani wa Sangabuye,Renatus Mulunga,alisema maendeleo ya ujenzi wa madarasa kwenye manispaa hiyo ni mazuri na kutahadharisha kila senti itafanya kazi iliyokusudiwa.
Baadhi ya wakuu wa wa shule za Kilimani (Gerena Majaliwa),Lukobe (Prosper Muyanja),Kisundi (Khalid Kazinja) na Shibula (Michael Paul) walieleza changamoto ya maji ya ujenzi na mabadiliko ya bei za baadhi ya vifaa vya ujenzi.