Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Staki Senyamle kuunda timu ya wataalamu kufanya mapitio ya thamani ya pesa ambayo imetumika katika ujenzi wa shule maalum ya msingi Mbuye kata ya Bwina Wilayani Chato.
Katibu Mkuu ametoa maagizo hayo tarehe 17 Novemba, 2021 alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 4.3 ambao ulianza mwezi Agosti, 2019 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2020, ukiwa mpaka sasa mradi umegharimu Shilingi bilioni 3.7 licha ya kuwepo na mapungufu mengi.
Ndg. Chongolo amemtaka Mkuu wa mkoa, aunde timu ya wataalam itakayojumuisha taasisi mbalimbali ikiwemo TARURA, TANROAD, TBA, Ofisi ya Mkuu wa mkoa, ofisi ya Mkuu wa wilaya na Halmashauri kufanya mapitio ya mradi kuona thamani halisi ya fedha ambazo zilitumika katika ujenzi wa shule maalum ya Mbuye.
Katibu Mkuu Ndg. Chongolo ametoa maagizo hayo kutokana na utekelezaji wa mradi huo kuonekana unasuasua na kuchukua muda mrefu huku ukiwa na mapungufu mengi yanayotia mashaka kuhusu thamani ya pesa na mradi unaoendelea kutekelezwa.