Kiongozi na Mtafiti Mkuu wa mradi kutoka SUA, Profesa Japhet Kashaigili akizungumza na viongozi wa vyama vya watumia maji wakati wa kuanza rasmi utafiti huo.
Bwana Siasa Shabani, Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji kwenye Mto Mbarali (JUWAMBA) akitoa neno kwenye kukao hicho.
Na Amina Hezron, Mbeya
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameanza rasmi kufanya utafiti wa tathimini ya maji na mazingira ya Mto Mbalali ili kusaidia Serikali katika kupanga mipango ya utekelezaji wa namna bora ya kuhifadhi mto huo wenye faida kubwa za kiuchumi kwa Taifa.
Akizungumza na viongozi wa vyama vya watumia maji wakati wa kuanza rasmi utafiti huo, Kiongozi na Mtafiti mkuu wa mradi kutoka SUA, Profesa Japhet Kashaigili amesema kuwa awamu hii ya kwanza ya utafiti huo unahusika na kuchukua sampuli na kufanya vipimo muhimu katika kipindi hiki cha kiangazi na baadae wataendelea kufanya hivyo kwenye misimu yote ya mwaka ili kukusanya taarifa muhimu zinazohitajika.
“Tunataka tusaidiane kuainisha maeneo ambayo yanahitaji utekelezaji wa kuanzia sasa. Nakumbuka kuna kipindi tuliweza kutembelea kitalu chenu cha miti tukakuta kile kitalu kimeharibika kutokana na kushindwa kuhudumiwa kama ambavyo ilipangwa. Hivyo, tutakaa pamoja tuangalie namna gani tuweze kukifanyia kazi, na tuainishe maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili tufanikishe kuyarudisha kwenye hali yake”, alifafanua Profesa Kashaigili.
Aliongeza “Kwakuwa swala hili ni la ushirikishi na jamii inayozunguka mto pamoja na vyombo vingine vya Serikali tutasaidiana katika kuwafikia walengwa. Na miongoni mwetu kama timu ya watafiti, baadhi yetu wataongea na jamii ili kupata takwimu sahihi kutoka kwa watumiaji wa maji; na wengine tutashirikiana kuchagua maeneo sahihi ya kuchukua sampuli na kufanya vipimo vya maji, mto na mazingira”.
Aidha, amesema kuwa wanajaribu kujua mto upoje kwa ujumla wake na tathimini hiyo haiangalii maji tu, wataangalia pia ikolojia ya mto kwani kuna viumbe hai ambavyo uwepo wao kwenye eneo fulani la mto au kukosekana kwao kunaashiria jambo fulani; hivyo kutahitajika msaada wa wakazi ambao wanajua maeneo hayo vizuri.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wengine wa jumuiya ya watumia maji, Bwana Siasa Shabani, Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji kwenye Mto Mbarali (JUWAMBA) amewapongeza watafiti hao kutoka SUA, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (UDSM),Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), na Ofisi ya Bonde la Mto Rufiji kwa kuamua kufanya utafiti huo ambao utawasaidia sana wao kama watumiaji wa maji kuweza kupata njia bora za kisayansi za kulinda mto huo.
“Tunashukuru na kufarijika sana kuona nyinyi kama watafiti mmeamua kufanya utafiti na tathimini hii muhimu kwa ustawi wa mto huu wa Mbarali na kubwa zaidi kuamua kufanya kazi kwenye maeneo ya mto moja kwa moja kuliko kuja na kuishia kwenye semina za ukumbini bila kujua hali halisi ya kile kinachoendela kwenye mazingira ya mto na bonde”, alieleza Bwana Siasa.
Utafiti huo wa miaka miwili ni moja kati ya miradi mitano inayotekelezwa katika nchi tisa kufikia malengo manne ya mradi mama mkubwa ambao unaitwa WIOSAP ambao malengo yake ni usimamizi wa makazi maalumu ya viumbe,kuboresha ubora wa maji ili ifikapo mwaka 2035 maji katika nchi hizo zinazotekeleza mradi huo yafikie viwango vya kimataifa usimamizi endelevu wa mtiriko wa mito na utawala na ushirikiano wa kikanda.