Mkuu wa Wilaya ya Magu,Salum Kalli (mwenye shati la kitenge),akielekeza jambo baada ya kushiriki kuwapanga machinga kwenye soko la Kona ya Kayenze na stendi mpya ya magari.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Isangijo, Malimi Patrick Pombe,akimwonyesha Mkuu wa Wilaya ya Magu,orodha ya wajasiriamali wa kijiji hicho kwa ajili ya kupangiwa maeneo ya biashara.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli,akizungumza na wafanyabiashara wadogo (machinga) wakti wa kuwapanga kwenye soko la Kona ya Kayenze, katika Kijiji cha Isangijo jana.
Wajasiriamali wanawake baadhi wakiwa wametandika khanga, vitenge na mitandao kwenye maeneo waliyopangiwa na serikali eneo la Kisesa Kona ya Kayenze.
Wananchi wakiwemo wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali wakisubiri kupangiwa maeneo ya biashara kwenye Soko la Kona ya Kayenze wilayani Magu jana. Picha zote na Baltazar Mashaka
………………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA,Magu
SERIKALI wilayani Magu,imewagawia maeneo wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo (Machinga) zaidi ya 2,600 ya kufanyia biashara na kuwataka kufanya biashara kwa uhuru na kujiepusha na uvunjifu wa amani.
Pia imeagiza wamiliki wa magari madogo ya abiria kutoa huduma ya usafiri hadi usiku ili kutoa fursa na kuepusha usumbufu kwa wafanyabiashara na wateja wao wanaporudi nyumbani baada ya kufunga Soko la Kona ya Kayenze.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, alitoa maagizo hayo jana baada ya kushiriki kuwapanga machinga kwenye soko la Kona ya Kayenze na kuahidi soko hilo litafanya kazi hadi saa 2:00 usiku ambapo serikali itaendelea kuliboresha na kulifanya la kisasa ili kukidhi mahitaji ya wafanyabiashara hao.
Alisema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwapanga machinga ni njema,inataka watambulike na kukopesheka kwenye taasisi za fedha ili wakuze mitaji na biashara zao hivyo waliokosa maeneo watatafutiwa ili pia wafanye biashara.
“Wananchi mliopata maeneo njooni mfanye biashara mtafute riziki halali,wala msidanganyike na wanaopanga kuvuruga amani kwa kisingizio cha kukosa nafasi Mungu atawalaani,pia utaratibu wa serikali kuwapanga kutoka kwenye maeneo yasiyo rasmi inataka kuona mnafanya kazi kwenye mazingira salama badala ya pembezoni mwa barabara,”alisema Kalli.
Alisistiza hakuna machinga atakosa eneo la biashara atahakikisha wote wanapata fursa hiyo na kuwataka waendelee kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kibiashara kwa sababu amedhamiria kuwainua na kuwawezesha kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya ya Magu,wapo machinga ziaidi ya 2,600 wakiwemo wauza nyanya,vitunguu,mboga mboga, matunda, nguo na bidhaa zingine ambapo zaidi ya 1,000 wamepangwa kwenye Soko la Kona ya Kayenze,wengine soko la Bujora na 150 katika soko la Nyanguge.
Mwenyekiti wa Shirika la Machinga Mkoa wa Mwanza (SHIUMWA),Mohamed Dauda, alisema zoezi hilo wilayani Magu limefanyika kwa ustaarabu na nidhamu ya hali ya juu na kumpongeza Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kusimamia kwa weledi na umakini wa hali ya juu lakini akasikitishwa na diwani mmoja kuwashawishi wananchi wagome kuhamia kwenye soko jipya.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Joseph Mwita, alisema wanafuatilia kuona na kuhakikisha watu wao wanapelekwa kwenye maeneo yanayostahili hali ambayo imesababisha shughuli nyingi kusimama,ingawa changamoto hazikosekani pale maisha ya binadamu yanapoguswa.
“Tunafuatilia kuona maagizo ya Rais Samia yametekelezwa au laa, tunataka tuone nidhamu imetumika,heshima, utu na utulivu kama ilivyofanyika Magu.Soko hili na maeneo mengine yataboreshwa zaidi kwa sababu ni ya kudumu,”alisema.