………………………………………………………….
NA MUSSA YUSUPH,MISSENYI
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christina Mndeme amewaomba wananchi kupuuza watu wanaopotosha suala la chanjo ya Uviko-19 pamoja na zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani.
Amesema Sensa ya Watu na Makazi itaiwezeshesha serikali kuandaa mipango ya kuhudumia wananchi katika maeneo yao kulingana na idadi ya wananchi.
Akizungumza jana na wananchi wa Kijiji cha Bulembo, Kata ya Kasheshe, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, alisema watu wanaopinga chanjo ya Uviko-19 na Sensa wanapaswa kuogopwa kwani hawalitakii mema taifa.
“Hata mama hawezi kupika chakula bila kujua idadi ya watu wake, kama akipika ndizi tano wakati watu waliopo ni sita hiyo haitawezekana. Mjitokeze kwa wingi kwa kila mtu kuhesabiwa. Tuwapuuze watu wanaojitokeza kuhamasisha watu wasichanje na kushiriki sensa,” alieleza.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina mapenzi mema na wananchi wake na ndio maana imekuwa ikitoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo.
“Rais Samia ametoa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Missenyi kwa sababu wakati wa kampeni alitoa ahadi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwamba CCM itaendelea kuboresha afya za wananchi kwa kujenga hospitali na vituo vya afya,” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu Bara.
Alibainisha kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya ni matokeo ya uchapakazi wa serikali ya Rais Samia katika kutatua kero za wananchi hususan sekta ya afya kwani itakuwa hospitali ya kwanza kujengwa na serikali tangu wilaya hiyo ilipoanzishwa mwaka 2006.
Kadhalika, aliuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) katika mwaka ujao wa fedha itenge fedha za ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa tano inayokwenda katika hospitali hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami.
“Katika kipindi hiki cha mvua, TARURA wanapaswa kuhakikisha barabara hii wanaikarabati kwa kiwango cha changarawe ili ianze kupitika na mwaka ujao wa fedha itengwe bajeti ya kuijenga kwa kiwango cha lami,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Waziri Kombo, alisema Juni mwaka huu walipokea fedha sh. milioni 500 za kuanza ujenzi wa hospitali hiyo.
Alisema hadi sasa sh. milioni 144.4 zimetumika huku sh. milioni 355 zikiwa bado hazijatumika katika mradi huo uliopangwa kukamilika Novemba 30 mwaka huu.