Mkurugenzi mtendaji wa chama Cha wazalishaji  wa mbegu Tanzania (TASTA)Baldwin Shuma akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano huo wa wadau wa mbegu uliofanyika mjini hapa (Happy Lazaro)
Mkurugenzi wa biashara kutoka kampuni inayohusika na kilimo na teknolojia ya Quincewood group Ltd,Fatma Fernandes akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha leo(Happy Lazaro)
Wadau wa mbegu wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa kilimo , Adolf Mkenda mara baada ya mkutano huo uliofanyika mjini Arusha (Happy Lazaro)
********************************
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Waziri  wa kilimo,Profesa  Adolf Mkenda amezitaka halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu ili wakulima waweze kupata mbegu bora za aina mbalimbali ya mazao ambazo zitazalishwa kwa wingi na kuwafikia kwa  urahisi wakulima ili waweze kulima  kilimo  chenye tija.
Waziri Mkenda ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa uzalishaji wa mbegu jijini Arusha ambapo amezitaka halmashauri za wilaya ambazo zinatoza ushuru wa kusafirisha mbegu za mazao kuacha mara moja kwani hakuna sheria inayo ruhusu kutoza ushuru wa mbegu.
Amesema kuwa ,kuanzia sasa serikali itayadhibiti makampuni ambayo yanazalisha mbegu za mazao mbalimbali zisizo na ubora lengo likiwa  ni kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na mbegu zote zitakuwa na lebo maalumu  ya kuonyesha ubora wake.
Waziri Mkenda amesema kuwa ,serikali itendelea kusimamia upatikanaji wa mbegu  bora za mazao  mbalimbali ili kuwezesha kuwepo kilimo chenye tija ambacho kinatoa mazao mengi na kusisitiza kwamba mageuzi ya kilimo  lazima yaanze na uzalishaji wa mbegu  bora.
Ameongeza kuwa , serikali itaongeza fedha za utafiti na uzalishaji wa mbegu bora sanjari na kusomesha vijana  kwenye vyuo mbalimbali mahiri duniani katika ngazi za masta na PHD kwa kuwa wataalamu waliopo wanastaafu.
Hata hivyo Waziri Mkenda ameziomba  benki nchini kuwekeza kwenye sekta ya kilimo  kutokana na kutambua kuwa changamoto inayoikabili sekta ya kilimo ni  upungufu wa fedha, hivyo benki zinayo nafasi kubwa ya kusaidia kuboresha kilimo nchini kwa kuwa kilimo kina faida.
Naye  Mkurugenzi mtendaji wa chama cha wazalishaji wa mbegu Tanzania  (TASTA) Baldwin Shuma , amesema kuwa,maeneo ya kuzalishia mbegu ni muhimu ili kutunza mbegu zinazopatikana hapa nchini na hiyo itazuia uigizwaji wa mbegu  nje ya nchi.
“Naziomba halmashauri kutenga maeneo ya kuzalisha mbegu kwani ni muhimu Sana na tusipofanya hivyo Sasa  hivi maeneo yatakuwa yameshajaa,hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunatenga maeneo ya kutosha ili kuendelea kuzalisha mbegu zaidi na kuweza kuwatosheleza wakulima wetu.”amesema Shuma.
Ameongeza kuwa, ni wakati sasa kama nchi kuongeza wawekezaji kutoka nje ili kuwekeza kwenye sekta ya mbegu ambapo sekta binafsi inaangalia ina mbegu za kutosha lakini pia wakulima kujitathimini kama wana mbegu na wao kama TASTA  wamejipanga vizuri .
Kwa upande wake  Mkurugenzi wa biashara  kutoka kampuni inayohusika na teknolojia na kilimo  ya Quincewood group Ltd ,Fatma Fernandes, amesema kuwa,  wameanzisha mfumo  wa mawakala wa sekta ya kilimo nchini unaowawezesha kununua na kuuza mbegu bora na kuweka kumbukumbu  za mauzo na mikopo waliyoitoa na wao wataichakata na kuiwasilisha serikalini.
Amesema  kuwa,mfumo huo umebuniwa kwa kushirikiana na AGRA na tayari wapo katika mikoa saba ambapo tayari mawakala 600 wameshajiunga na mfumo huo ambao unarahisisha  mbegu kumfikia mkulima hivyo mfumo huo ni mkombozi , huku lengo likiwa ni kuhakikisha mfumo huo unaenea nchi nzima.