Chifu wa kabila la Wangoni kutoka Songea Emmanuel Zulu Gama kulia akitoa damu jana kwa ajili ya kupima afya wakati wa kampeni ya uibuaji wa ugonjwa wa kifua kikuu katika kijiji cha Kidodoma wilaya ya Tunduru, kushoto ni mtaalam wa maabara kutoka shirika lisilo la kiserikali ya MDH Anna Enock
Muuguzi wa Zahanati ya Kidodoma wilaya ya Tunduru Elice Makumbuli akitoa chanjo ya Corona kwa mkazi wa kijiji hicho Yasin Tawala wakati wa zoezi la utoaji chanjo ya Uvico-19 linaloendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Chifu wa kabila la Wangoni kutoka Songea Emmanuel Zulu aliyevaa mavazi rasmi ya Kichifu akiwaongoza baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kidodoma wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kwenda kuchanja chanjo ya Covid 19 baada ya kumalizika kwa maombi ya kuliombea Taifa kuhusu ugonjwa huo,kulia Diwani wa Kidodoma Shaban Nyenje.
*****************************
Na Muhidin Amri,
Tunduru
KIONGOZI wa kabila la Wayao wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Said Mussa (Sultani Mataka) machifu na viongozi wa jadi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma wamekusanyika katika kijiji cha Kidodoma wilayani humo kwa ajili ya kufanya maombi ya kuliombea Taifa kuhusu ugonjwa wa Covid-19.
Sultani Mataka alisema, wamelazimika kufanya maombi maalum kwa Mwenyezi Mungu ili ainusuru nchi yetu na ugonjwa huo ambao unaendelea kupoteza maisha ya Watanzania wengi na kupunguza nguvu kazi ya Taifa.
Kiongozi huyo wa kabila la Wayao, amewaomba Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo na kujitokeza kwa wingi kupata chanjo katika vituo vilivyotengwa na Serikali.
Aidha Sultani Mataka, amewataka wananchi kuzingatia maelekezo na ushauri unaotolewa na wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka,kuvaa barakoa na kutumia vitakasa mikono.
Alisema, kila mwaka wanafanya maombi ya kuliombea Taifa kulingana na tatizo lililopo na kabla ya maombi wanakwenda kwenye makabauri ya Mababu zao kwa ajili ya kupata baraka ambazo kwa imani za kabila la Wayao zinasaidia kufanikisha mahitaji na shida zao.
Mwenyekiti wa viongozi wa jadi wa wilaya ya Tunduru Issa Malungusya alisema, kila mwaka Sultani,Machifu na viongozi wa jadi wanakutana nyumbani kwa Sultani Mataka kwa ajili ya maombi maalum kuhusiana na shida na jambo lililo mbele yao ili Mwenyezi Mungu aweze kuwanusuru.
Alisema, kwa sasa hali ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo hapa nchini sio nzuri licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali,hivyo wana amini mwenye uwezo wa kumaliza tatizo la Corona ni Mungu.
Amewataka wananchi hasa wakazi wa wilaya ya Tunduru, kuendeleza mira na utamaduni wa kabila lao kwani hatua hiyo inasaidia sana kupunguza na hata kutokomeza baadhi ya majanga yanayojitokeza katika jamii badala ya kukumbatia utamaduni kutoka nje.
Naye Chifu wa kabila la Wangoni kutoka Songea Emmanuel Zulu Gama amefurahi kushiriki katika maombi hayo ili kwa pamoja wamuombe Mungu aweze kuisaidia Nchi yetu kutokomeza ugonjwa huo ambao unaendelea kupoteza maisha ya wananchi wengi
Chifu Zulu Gama,amewaomba Watanzania kujithamini na kuwa waangalifu kwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo na magonjwa mengine na kuepuka tabia ya kupuuza ushauri unaotolewa na wataalam wa Afya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru Dkt Wendy Robert alisema,mwitikio wa Wananchi kujitokeza kupata chanjo ya Corona ni mkubwa na kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya afya itaendelea kupeleka chanjo katika maeneo yote.
Amewataka wananchi wa wilaya hiyo,kuchangamkia kupata chanjo na kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ili kuwa na uhakika wa afya zao.
Kwa mujibu wa Dkt Wendy,wilaya ya Tunduru imejipanga kuhakikisha maeneo yote yanakuwa na chanjo za kutosha na hakuna mwananchi atakayekosa huduma hiyo ambayo inatolewa bure na wahudumu wa afya.