Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza katika Kikao cha Mawaziri wa Sekta zinazotekeleza Mpango wa Lishe kilichofanyika Novemba 10, 2021 katika Ukumbi wa mkutano katika Ofisi hiyo Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Mwanaidi Khamis (kulia) akimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa kikao hicho. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi. Nadhifa Kemikimba.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu akieleza jambo wakati wa mkutano huo. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Sera na Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Paul Sangawe akiwasilisha Mkakati wa Serikali katika kuboresha Lishe nchini wakati wa Kikao hicho cha Mawaziri wa Sekta zinazotekeleza Mpango wa Lishe kilichofanyika Novemba 10, 2021 katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Ngome, Jijini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akichangia jambo wakati wa mkutano huo.
*************************
Na: Mwandishi Wetu – DODOMA
Mawaziri sekta zinazotekeleza Mpango wa lishe wamekutana leo Novemba 10, 2021 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kujadili na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Mwaka wa Wadau wa Lishe utakaofanyika Mkoani Tanga.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa mkutano huo kwa kushirikiana na Wizara zinazotekeleza mpango wa lishe pamoja na wadau wa lishe (Joint Multisectoral Nutrition Review) kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya lishe pamoja na mikakati ya Serikali katika kupunguza changamoto ya utapiamlo nchini.
“Suala la lishe ni mtambuka linalosimamiwa kwa ujumla wet una mkitizama sekta ambazo zipo hapa zinaguswa moja kwa moja kwenye suala hili la lishe bora na kupambana na udumavu, utapiamlo na mambo mengine yanayohusu lishe,” alisema Waziri Mhagama
Alifafanua kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu katika kufanikisha hayo imekamilisha maandalizi ya Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Pili wa Masuala ya Lishe (2020/21-2025/26) ambao utatoa mwongozo wa utekelezaji wa afua za lishe hapa nchini kwa miaka mitano.
Waziri Mhagama aliongeza kuwa, Mkutano huo wa mwaka utafanyika Mkoani Tanga kwa lengo la kuhamasisha wananchi wa mkoa huo kuongeza jitihada katika masuala ya lishe na hivyo kurudisha mkoa huo katika nafasi iliyokuwa awali na ikiwezekana kufanya vizuri zaidi.
“Zamani mkoa wa Tanga ulikuwa unafanya vizuri kwenye masula ya lishe lakini hivi karibuni imeonekana kuwa na kiwango cha udumavu katika masuala ya lishe, hivyo mkoa huu unahitaji uhamasishaji wa hali ya juu katika masuala ya lishe ili kuwa ni moja ya Mikoa ambayo itakuwa kielelezo cha mafaniko katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Pili wa Masuala ya Lishe,” alisema Waziri Mhagama
Sambamba na hayo, Mheshimiwa Mhagama alipongeza juhudi zilizochukuliwa katika kusimamia mapambano dhidi ya utapiamlo ambapo alieleza jitihada hizo za wazi zitawezesha kufikia malengo waliyojiwekea katika kupunguza viwango vya utapiamlo nchini.
Pia alipongeza mchango na juhudi katika kuimarisha masuala ya lishe ikiwemo sekta ya Kilimo kwa kuandaa Kilimo kwa Mpango Mkakati wa Kujumuisha Masuala ya Lishe kwenye Kilimo ambao utasaidia kuimarisha uratibu wa sekta ya kilimo katika kupambana na utapiamlo nchini. Upande wa sekta ya Afya ni kuratibu maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa ambayo hutumika kutoa uelewa wa masuala ya lishe kwa jamii. Pamoja na kuandaa Mkakati wa Kupambana na Magonjwa yasiyoambukiza ambao utazinduliwa hivi karibuni. Upande wa sekta ya Elimu ni uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimu ya Msingi ambao una lengo la kuwawekea watekelezaji na wadau wa utoaji wa huduma hiyo ya chakula na lishe shuleni namna bora ya kutekeleza, kusimamia na kuboresha utoaji wa huduma hiyo nchini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Prof. Jamal Katundu alisema kuwa, Tanzania ni nchi mwanachama wa Vuguvugu la Lishe Duniani “Scaling Up Nutrition (SUN) Movement”, kama taifa lilipokea mwaliko wa kushiriki katika Mkutano huo wa Wadau wa Lishe wa Mwaka 2021 unaojulikana kama Nutrition for Growth Summit (N4G) utakaofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 7 na 8 Desemba 2021, Tokyo – Japan.
“Katika kuhakikisha nchi yetu inashiriki kikamilifu kwenye mkutano huo, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau imeratibu maandalizi ya ushiriki huo kwa kuandaa maeneo ambayo Nchi yetu itaahidi kutekeleza katika kipindi cha Miaka Mitano ijayo,” alisema Naibu Katibu Mkuu Prof. Jamal
Mkutano huo wa Mawaziri Sekta zinazotekeleza Mpango wa Lishe umependekezwa kufanyika tarehe 17 hadi 18 Novemba, 2021 Mkoani Tanga na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Kassim Majaliwa (Mb). Kauli mbiu ya mkutano huo ni; “LISHE BORA NI MSINGI WA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU KATIKA UCHUMI SHINDANI”.